DESEMBA 15,2021 JUMATANO: JUMA LA 3 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Isa 45:6-8, 18-25
Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kuihuluku giza; mimi nafanya suluhu na kuhuluku ubaya; mimi ni Bwana niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu yamwage haki; nchi na ifunuke ili kutoa wokovu, nayo itoe haki ikemee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba. Maana Bwana aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, Mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia. Kwa Bwana, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkadirikia watatahayarika. Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

WIMBO WA KATIKATI:Zab 85 :8a, 9-13

1.Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Dondokeni, enyi mbingu, toka juu,
Mawingu na yamwage haki.
2.Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana,
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
3.Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

INJILI: Lk 7:19-23
Siku ile Yohane aliwaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu, akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohane Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.

TAFAKARI
TUSIMAME KATIKA UKWELI: Yohane Mbatizaji kama Wayahudi wengine alikuwa anamngojea Masiha kwa hamu kubwa. Akiongozwa na utabiri wa nabii Isaya 61:1-2, anasikia mambo aliyokuwa anayafanya Yesu yaliashiria kuwa ndiye Masiha. Anamwuliza Yesu kama ndiye au waendelee kusubiri. Yesu anampa kazi ya kwenda kufanya yaani kutangaza aliyoyaona na kusikia, kuwa vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wagonjwa wanaponywa, wakoma wanatakasika, wafu wanafufuliwa na maskini wanatangaziwa Habari Njema. Tunafika katikati ya kipindi hiki cha Majilio. Yesu ametutendea haya yote yaliyoainishwa hapa. Tujiandae vema kumpokea katika maisha yetu. Tutengeneze njia ya kumwezesha Masiha kupita na tufungue kufuli za mioyo yetu ili apate kuingia. Tusisubiri kama watu ambao hawajaonja uwapo wa Masiha katika maisha yao. Matendo yetu yashuhudie kweli kuwa sisi tuliobatizwa tayari tumeonja uwapo wa Masiha katika maisha yetu. Maisha yetu sisi Wakristo yawaguse watu nao wapate matumaini mapya.

Sala: Ee Yesu mnyenyekevu, naomba neema ya kutangaza makuu yako.