DESEMBA 14,2021 JUMANNE:JUMA LA 3 LA MAJILIO

Mt. Yohane wa Msalaba, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Sef 3:1-2, 9-13
Bwana asema: Ole wake yeye aliyeasi na kutia unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya kuishi; waliombao sua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hatutatahayarika matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.

WIMBO WA KATIKATI Zab:34:1-2, 5-6, 16-17, 18, 22

1.Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia.
2.Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zao zote. (K)
3.Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
4.Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)

INJILI: Mt 21:28-32
Siku ile, Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee: Mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohane alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini; nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

TAFAKARI
MATENDO YANANENA KULIKO MANENO: Katika Injili tumemsikia Yesu akitoa mfano wa watoto wawili wa baba mmoja wanaotumwa kwenda kufanya kazi shambani. Wa kwanza anampa baba yake matumaini ya uongo kwani hajatimiza haja ya baba yake. Wa pili anakataa ila katika tafakari anagundua kamkosea baba yake hivyo anaenda shambani na kutekeleza matakwa ya baba yake. Huyu anasifiwa na wale waliokuwa wakimsikiliza Yesu. Tupo katika ulimwengu ambao una watu wa mtazamo wa mtoto wa kwanza ambao wanadhani kwa kuitikia mwaliko wa Mungu tu bila kuufanyia kazi tayari wamepata wokovu. Wapo mstari wa mbele kuwashambulia walioko upande wa yule mtoto wa pili ambaye alionesha kukataa. Kimsingi huyu alikataa kwa maneno tu lakini kwa matendo alikuwa mtii kwa baba yake. Mtoto wa pili ni mfano wa mtu mwenye toba ya kweli. Tusimdanganye Mungu na watu kwa maneno yetu bali tuweke katika matendo maagano yetu ya ubatizo ili Mungu atukuzwe nasi tupate utakatifu.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, naomba imani yangu iakisi matendo yangu ya kila siku.