Mt.Lusia,Bikira na Shahidi
Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Hes 24:2-7, 15-17
Siku zile Balaamu aliinua macho yake akawaona Israeli, wamekaa kabila kabila, roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, yeye aonaye maono ya Mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; mahema yako ni mazuri namna gani, ee Yakobo, maskani zako, ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, mfano wa bustani kando ya mto, mfano ya mishubiri aliyoipanda Bwana, mfano ya mierezi kando ya maji. Maji yatafurika katika ndoo zake, na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake atadhimishwa kuliko Agagi, na ufalme wake utatukuzwa.
Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Biori asema, yule mtu aliyefumbwa macho asema, asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, na kuyajua maarifa yake aliye juu. Yeye aonaye maono ya mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, namwona, lakini si sasa; namtazama, lakini si karibu; nyota itatokea katika Yakobo; na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli.
WIMBO WA KATIKATI:Zab 25:4-6, 7b-9
1.Ee Bwana, unijulishe nja zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.
2.Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. (K)
3.Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole akawaongoza katika hukumu
Wenye upole atawafundisha njia yake.
INJILI: Mt 21:23-27
Siku ile Yesu alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu, akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizao wa Yohane ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?
Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohane kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia
TAFAKARI
CHANGAMOTO KATIKA MAISHA YA UFUASI: Yesu katika utume wake alitenda mengi mema ambayo yaliwavuta wengi wamwelekee Mungu. Kutokana na uwezo aliokuwa nao na mtazamo mpya aliokuwa nao alipata upinzani kutoka kwa watu wake na viongozi wa wakati wake, lengo likiwa ni kumkwamisha. Walitaka kujua ni kwa amri ya nani anatenda makuu aliyotenda. Yesu aliwajibu kwa kuwauliza swali ambalo kama wangejibu ingekuwa wanajipinga wenyewe na hivyo wanakwepa na wanakuwa waongo kwa nafsi zao. Ni katika hali kama hiyo tunaweza kusema katika ukweli uongo hujitenga. Neno hili litufundishe kuwa tuwe wakweli kwa nafsi zetu hata kama ukweli utatugharimu sadaka kubwa. Tuusimamie ukweli tuutunze ukweli na kuulinda ukweli kila wakati. Tuwe na hekima, busara na werevu katika kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo katika maisha ya ufuasi. Tusiogope changamoto bali zitufanye tuwe na bidii zaidi. Yesu hakurudi nyuma kwa sababu ya changamoto.
Sala: Ee Yesu Mkombozi wangu, naomba unijalie uvumilivu katika maisha ya kukufuasa.