DESEMBA 12,2021 DOMINIKA:DOMINIKA YA 3 YA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Sef 3:14-18
Imba, Ee binti Sioni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sioni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako.

WIMBO WA KATIKATI:Isa. 12:2-6

1.Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu.
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu.
(K) Paza sauti, piga kelele maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
2.Mshukuruni Bwana, liiteni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
3.Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

SOMO 2: Flp 4:4-7
Ndugu zangu: Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

INJILI: Lk 3:10-18
Siku ile: Makutano wakamwuliza Yohane Mbatizaji, Tufanye nini basi? Akawajibu akawaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu. Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohane, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini anakuja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuulegeza ukanda wa viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.

TAFAKARI
FURAHINI KATIKA BWANA: Dominika ya tatu ya Majilio huitwa pia Dominika ya furaha. Masomo yetu hugusia furaha hii. Maneno ya wimbo wa mwanzo yanatualika tufurahie katika Bwana. Maneno haya tunayakuta tena katika somo la pili. Ni maneno aliyosema mtume Paulo kwa kanisa la Filipi. Ni Kanisa lililokuwa na ukarimu sana kwa Paulo katika uenezaji wa Injili na Paulo alilipenda sana. Leo anaongea nao kirafiki kama watu walio katika imani kubwa wakimsubiria Bwana Yesu arudi kwao na hakika angaliwapatia tuzo kubwa kwani walikuwa Kanisa aminifu kwa Kristo. Paulo anawataka wabakie katika matumaini kila wakati. Wakipatwa na shida wamweleze Bwana, na wabakie kuwa watu wa shukrani, kusali na kuomba kila wakati. Huu ni ujumbe wa matumaini kwetu; yatupasa tubakie katika uaminifu na matumaini katika wajibu wetu na maisha yetu kama Wakristo. Wakristo wa Filipi walisifika kwa uaminifu na ukarimu. Nasi tuige tunu hizo.
Maneno ya wimbo wa katikati yanatoka katika kitabu cha nabii Isaya 12. Huu ni wimbo wa ukombozi na maneno yake yanafanana na ule wimbo aliouimba Musa na wana wa Israeli baada ya kuvuka Bahari ya Shamu salama (Kut 15). Leo tunatumia maneno haya kushangilia tendo la Mungu la ukombozi la kumtuma Mwanae wa pekee kutukomboa. Tunayo kila sababu ya kufurahi. Tuwe tayari kupeleka furaha hii kwa wenzetu pia. Kila tulipo tutangaze amani na furaha, tusifiche furaha zetu, tusitake tufurahi sisi mwenyewe tu. Tuwashirikishe wenzetu kile kinachotupatia furaha.
Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Sefania linatualika kufurahi pia. Tunasoma, “Furahi ewe binti Sioni, piga kelele,” kwa sababu Bwana amemtupa nje mtesi wa Israeli. Israeli aliangushwa na dhambi za uasherati na kuabudu sanamu (2Fal 24). Lakini sasa ataupata ukombozi. Ukombozi uliwaletea Israeli matumaini makubwa. Uliwarudishia Israeli hadhi yao ya kuwa wana wa Mungu waliyoipoteza kutokana na ukaidi wao.
Nasi tunahitaji ukombozi; ukombozi huanza kwa sisi kusamehewa makosa yetu na Bwana. Dhambi humwangusha mwanadamu na kumrudisha katika utuMwa Hivyo ukombozi huanza kwa sisi kuzitambua dhambi zetu na kuzikiri mbele ya Baba na kupata maondoleo ya dhambi. Sisi tusiache kuziungama dhambi zetu. Pia ukombozi unapaswa kutufanya tuishi katika amani na wenzetu. Bila amani, tutaishi katika hofu. Hatuwezi kusema kwamba tumepata ukombozi ikiwa tunaishi katika hofu bado.
Katika Injili, Yesu ameorodhesha namna ya kupeleka furaha ya ukombozi kwa wenzetu. Yohane Mbatizaji anapowabatiza askari na watoza ushuru, hawapi maagizo ya kuzikimbia kazi zao. Anawataka wazitakatifuze ajira zao na kuzitumia kuwapatia wenzao huduma. Hapa tunajifunza ujumbe mkuu kwetu kama Wakristo. Ukweli ni kwamba wengi wetu tumeshindwa kuzitakatifuza ajira zetu. Tumekuwa watu wa kuiga tabia zisizokuwa na uaminifu na kuruhusu rushwa kutawala ndani ya ajira zetu. Yohane Mbatizaji anatutaka kuzitakatifuza ajira zetu na kuzifanya zitoe huduma kwa wenzetu. Yohane Mbatizaji alipendelea mabonde ndani ya moyo wa mwanadamu yafunikwe kwa kuwa na mawazo yenye mtazamo wa namna hii.
Kwa nyakati zetu tunaalikwa pia kuitakatifuza mitandao yetu mbalimbali ya kijamii kwa kutuma habari zenye mafundisho na maadili mbalimbali katika mitandao hii. Tusishiriki katika kutuma habari zenye maadili mabaya katika mitandao hii. Mitandao ya kijamii yaweza kutumika vyema katika kushirikishana neno la Mungu na kushauriana vyema. Tujitahidi katika hili.
Yohane Mbatizaji aliwataka watoza ushuru na askari kuacha baadhi ya tabia zao mbaya ili waweze kupata wokovu. Nasi tunapaswa kutambua kwamba yapo mambo tupaswayo kuacha ili tuweze kuupata wokovu. Watoza ushuru waliambiwa waache kutoza ziadi ya ilivyokuwa inatakiwa. Sisi tujichunguze ni wapi tunapotoza vitu zaidi ya vinavyotakiwa? Kwa vyovyote, sisi sote tunapaswa kuacha madhaifu yetu kama, lugha chafu, uchochezi, uchoyo, ulevi, uasherati na ulafi.

Sala: Bwana, nisaidie niweze kukuona wewe kama ulivyo, na kuruhusu uwapo wako duniani uingie katika maisha yangu.