DESEMBA 11,2021 JUMAMOSI: JUMA LA 2 LA MAJILIO

Mt. Damasi I, Baba Mtakatifu
Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 48:1-4, 9-11
Ndipo aliposimama nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli. Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.

WIMBO WA KATIKATI Zab 80:1-2, 14-15,17-18

1.Wewe uchungaye Israeli, usikie,
Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na manase,
Uziamshe nguvu zako,
Uje utuokoe.
(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe,
Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.
2.Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule uliopanda
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya
Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)
3.Mkono wako na uwe juu yake
Mtu wa mkono wako wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya
Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. (K)

INJILI: Mt 17:10-13
Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu wakisema: Kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote; ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao. Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohane Mbatizaji.

TAFAKARI
KUKUTANA NA MUNGU: Nabii Eliya anajulikana sana na aliheshimika sana katika Agano la Kale. Alikuwa mcha Mungu sana na Mungu alimkirimia uwezo mkubwa katika utendaji wake. Katika tukio la Yesu kugeuka sura katika mlima mrefu, Musa na Eliya wanasikika wakizungumza na Yesu. Yesu aliwakataza mitume wake wasieleze kuhusu maono hayo. Pamoja na sauti na wazo la Petro la kumjengea kibanda bado wanafunzi wanang’ang’ania ujio wa Eliya. Hapa inaonekana wazi kuwa hata wao bado hawajamtambua Yesu pamoja na kuishi nao. Sisi wabatizwa tusiwe wagumu wa kutambua uwapo wa Mungu kati yetu. Katika maisha yetu ya sasa tujihadhari pia na wale wanaojiita manabii ila wana mkakati binafsi wa kupata kipato. Wapo Wakristo wengi wanaowakimbilia hasa wanapodanganywa wana uwezo wa kufanya miujiza fulani. Lakini pia tuwe manabii sisi kwa sisi katika maisha yetu sehemu mbalimbali kwa kufundishana ukweli wa kimungu.

Sala: Ee Mungu mwema, naomba unyenyekevu niwapokee wanaotoka kwako.