DESEMBA 10,2021 IJUMAA: JUMA LA 2 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Isa 48:17-19
Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi: Mimi ni Bwana Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari; tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 1:1-4, 6

1.Heri mtu Yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki,
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K)Akufuataye, Bwana, atakuwa na nuru ya uzima.
2.Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji.
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
3.Sivyo walivyo wasio haki,
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

INJILI: Mt 11:16-19
Siku ile, Yesu aliwaambia makutano: Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema, Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.
Maana Yohane alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo. Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.

TAFAKARI
TUTENGENEZE UPYA UHUSIANO WETU NA MUNGU: Wapendwa familia ya Mungu katika Injili ya leo Yesu anawashangaa wazee na viongozi wa Kiyahudi kukataa kujifunza kutokana na mwaliko wa Mungu kuwakumbusha watengeneze upya mahusiano yao na Mungu kwa njia yoyote. Yohane Mbatizaji aliwaendea na wazo la toba kali iliyooneshwa naye mwenyewe kwa kujinyima vyakula vizuri na vinywaji. Matokeo yake wamembeza na kusema, “Ana pepo mbaya” (Mt 11:18b). Yesu amekuja na sera yake ambayo ni shirikishi iliyoambatana na kuwa karibu sana na wanyonge wa taifa ili aweze kuwapata na kuwarudisha katika mstari ulionyooka. Hukumu ikatolewa dhidi yake kuwa ni mlafi, mlevi, rafiki wa watoza ushuru ambao walikuwa maadui wa watu pia rafiki wa wakosefu. Nabii Isaya anawakumbusha maagizo ya Mungu na baraka zitakazofuatana na kushika maagizo hayo kwa vizazi vyao. Tujitahidi kutokuwa na mioyo migumu na tuwe tayari kuonywa. Kwa kuyashika maagizo ya manabii na mitume na Yesu tutarudisha mahusiano yetu na Mungu yawe mazuri zaidi.

Sala: Ee Yesu mpendwa wangu, naomba unijalie ari ya kumtafuta Mungu na kuwa karibu naye.