Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: Isa 41:13-20
Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji. Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; ili waone, na kujua wakafikiri, na kufahamu pamoja; ya kuwa mkono wa Bwana ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.
WIMBO WA KATIKATI Zab:145:1, 9-13
1.Ee Mungu wangu, Mfalme nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
2.Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi,
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)
3.Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
INJILI: Mt 11:11-15
Siku ile, Yesu aliwaambia makutano: Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohane Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohane. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja. Mwenye masikio, na asikie.
TAFAKARI
TUDHIHIRISHE UTEULE WETU KWA MATENDO: Katika somo la kwanza tumemsikia nabii Isaya akiwatuliza watu waliokuwa wamekata tamaa. Anawapa matumaini mapya kuwa mateso yao yataisha kwani Bwana anawapenda kama taifa teule na ataendelea kuwalinda. Pamoja na hakikisho hilo la Mungu kwa taifa teule, katika Injili ya leo Yesu anatoa tahadhari kuwa tusitosheke kuwa taifa teule la Mungu kwa njia ya ubatizo tu. Tunapaswa kudhihirisha kwa matendo uteule wetu na msimamo wetu kwa Mungu. Anatuambia, “Tangu siku za Yohane mbatizaji hata sasa, ufalme wa Mbingu hupatikana kwa juhudi tu nao wenye juhudi ndio wanaounyakua” (Mt 11:12). Tunapokuwa katika kipindi hiki cha Majilio tuombe uvuvio mpya tuweze kuamsha ndani yetu yale yanayompendeza Mungu. Tuzingatie hasa mwaliko anaotupa Mtakatifu Yohane “Lakini nina tatizo nawe, umeacha upendo wako wa kwanza. Kumbuka ni kutoka wapi ulikotetereka. Tubu na kufanya tena matendo yako ya kwanza” (Ufu 2:4-5a).
Sala: Ee Mungu wangu, naomba ari ya kuendelea kuutafuta ufalme wako kwa matendo.