DESEMBA 4,2021 JUMAMOSI: JUMA LA 1 LA MAJILIO

Mt. Yohane wa Damasko, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa 30:19-21, 23-26
Bwana Mungu Mtakatifu wa Israeli asema: watu watakaa katika Sioni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.
Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.
Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ome zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa
ungo na kwa pepeo.
Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

WIMBO WA KATIKATI:Zab. 147:1-6

1.Msifuni Bwana, maana ni vema kumwimbia Mungu wetu
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
(K) Heri wote wamngojao Bwana.
2.Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi ya nyota,
Huzipa zote majina. (K)
3.Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu.
Akili zake hazina mpaka,
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri. (K)

INJILI: Mt 9:35 – 10:1, 6-8
Siku ile: Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.
Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.
Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.
Akawaambia, afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

TAFAKARI
HURUMA YA MUNGU KWA WATU WAKE: Katika somo la kwanza leo nabii Isaya anawaliwaza waliokuwa na majonzi. Anawapa matumaini ya kupata mahitaji yao. Kwa faraja hii wanapata tiba ya majeraha ya taifa lao na kuponywa makovu ya vidonda vyao. Anawatangazia maendeleo ya baadaye ikiwa ni pamoja na hali nzuri ya hewa, kupata malisho na kadhalika. Utabiri huu unajidhihirisha katika Injili Yesu mwenyewe anapowatangazia Injili ya ufalme anawaponya magonjwa yote na udhaifu wote. Anaandaa watu wa kuendeleza kazi aliyoanza yeye mwenyewe. Aidha, Yesu anawapa mamlaka na majukumu makubwa ikiwa ni pamoja na kuponya watu, kufufua wafu, kutakasa na kufukuza pepo. Huduma hizi zifanyike kwa ukarimu wa kimungu. Leo tunashuhudia watu wanaojiita manabii wakiigiza kufanya miujiza ila kwa lengo la kupata malipo fulani. Hiyo ni ishara wazi kuwa hajatumwa na Mungu. Tusiwape nafasi katika maisha yetu. Yesu hakuhitaji malipo kwa huduma yoyote aliyofanya na hakuagiza malipo yafanyike.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, nijalie moyo wa kujitoa sadaka bila kudai malipo.