DESEMBA 3,2021 IJUMAA: JUMA LA 1 LA MAJILIO

Mt. Fransisko Ksaveri, Padre
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa 29:17-24
Bwana Mungu asema: je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kuwa kitu kisichofaa. Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake. Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung’unikao watalifunza elimu.

WIMBO WA KATIKATI :Zab 27:1, 4, 13-14

1.Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru na wokovu wangu.
2.Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
3.Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

INJILI: Mt 9:27-31
Siku ile: Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema , Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipafu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.

TAFAKARI
IMANI YA KWELI INALIPA: Katika somo la kwanza nabii Isaya anawapa matumaini wale waliokata tamaa waendelee kumwamini Mungu. Waovu na wakandamizaji wataondolewa na hivyo amani na usitawi vitatawala katika nchi. Katika Injili tumesikia imani waliokuwa nayo vipofu waliomwendea Yesu wakiwa na imani ya kuponywa naye. Cha ajabu hawa vipofu hawakuwahi kumwona Yesu kwa macho yao kabla ya kuponywa, walisikia tu habari zake wakamwamini. Katika maisha yetu ya ufuasi yapo mambo kadhaa yanayoweza kudhoofisha imani yetu kwa Mungu. Tusiruhusu mkato wa tamaa hata mara moja bali tuendelee kumwamini Yesu. Tuna bahati ya kukutana naye kila mara katika Ekaristi Takatifu na neno lake. Tumpokee kwa imani kubwa na kulishika neno lake kwa imani kubwa kwani yeye ndiye mweza. Tuamini uwapo wake na nguvu iliyopo katika Ekaristi Takatifu tunayopokea kila mara. Ekaristi Takatifu inaponya maradhi ya roho na ya mwili pale tunapoipokea kwa imani na tukiwa na neema ya utakaso.

Sala: Ee Yesu naomba utuongezee imani.