DESEMBA 2,2021 ALHAMISI JUMA LA 1 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa 26:1-6
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Wekeni wazi malango yake, taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini Bwana siku zote, maana Bwana Mungu ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, mji ule ulioinuka, aushusha, aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, naam, miguu yao walio maskini, na hatua zao walio wahitaji.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 118:1, 8-9, 19-21, 25-27a

1.Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema
Kwa maana fadhili zake ni za milele
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wanadamu
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wakuu.
(K)Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana.
2.Nifungulieni malango ya haki
Nitaingia na kumshukuru Bwana.
Lango hili ni la Bwana,
Wenye haki ndio watakaoliingia.
Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
Nawe umekuwa wokovu wangu. (K)
3.Ee Bwana, utuokoe, twakusihi,
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi,
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu
Naye ndiye aliyetupa nuru. (K)

INJILI: Mt 7:21, 24-27
Siku ile, Yesu akawaambia wafuasi wake: Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

TAFAKARI
MASHARTI YA KUSHIRIKI KARAMU YA MBINGUNI: Wapendwa familia ya Mungu Injili ya leo inatualika tuweke katika matendo yale tunayoamini katika maisha yetu ya ufuasi. Kuwa na imani ya maneno tu haitatufikisha mbinguni. Kutekeleza mapenzi ya Mungu kunafananishwa na kujenga nyumba juu ya msingi imara ambao hata katika shida utabaki imara. Kufanya mapenzi ya Mungu ni kuishi anachosema nabii Isaya mtumainini Bwana siku zote maana Bwana Mungu ni mwamba wa milele. Tujihoji wenyewe kama imani yetu kwa Yesu ni imara au ni hafifu. Penye uimara tujitahidi kupaimarisha zaidi na penye udhaifu tuombe neema ya kupatengezeza vizuri. Haya yatawezekana endapo tutaweka katika matendo yale tunayoamini. Tukumbuke kuwa matendo yanaongea kwa sauti kubwa zaidi kuliko maneno matupu. Tupo katika ulimwengu ambao tunapaswa kumwungama Kristo na kumtangaza kwa matendo yetu mema.

Sala: Ee Yesu uliyekubali kutukomboa, nijalie kumtangaza Mungu kwa matendo yangu.