MT. ANDREA, MTUME
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Rum 10:9-18
Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:1-4
1.Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
2.Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.(K)
INJILI: Mt 4:18-22
Yesu alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata; Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
TAFAKARI
KUACHA YOTE NA KUMFUATA YESU:Katika Injili ya leo tumesikia mwito wa wanafunzi wa kwanza. Wote walioitwa walikuwa kwenye shughuli zao za kawaida. Yesu anapowaita wanaacha yote wanamfuata yeye. Yesu anapowaambia, “Nifuateni”, anatuambia tuende kwake na anatufungulia njia ya kwenda. Hawa wanafunzi walipokea mwaliko wakamfuata Yesu. Mtakatifu Andrea ambaye ni mmoja wa walioitwa alimfuata Yesu kwa uaminifu mkubwa akakubali kumwaga damu yake kwa ajili ya Kristo ndiyo maana leo tunasherekea ushindi wake. Tulipobatizwa tuliitikia mwaliko tuliopewa. Tudumu katika kumfuata kwa kuweka pembeni nyavu za masengenyo, hasira, wivu, wizi uasherati malimwengu na yote yanayoweza kuwa kikwazo katika kuitikia mwito wa Kristo. Hawa mitume walivyoitwa wakaacha vyote, hawakurudi nyuma kuchukua yale waliyoacha. Tulipobatizwa tulikubali kuacha mambo mengi sana tulipokiri imani kwa kuulizwa na padri. Tusirudie tena yale tuliyoyaacha na tusichanganye maisha mapya na ya kale. Divai mpya iendelee kubaki kwenye viriba vipya.
Sala: Ee Yesu wangu, nijalie kujiachanisha na malimwengu.