NOVEMBA 29,2021 JUMATATU: JUMA LA 1 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa 2:1-5
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amosi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sioni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingile, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

WIMBO WA KATIKATI:Zab 122:1-4, 8, 9

1.Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia,
na twende nyumbani kwa Bwana.
2.Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ule ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)
3.Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
Nikutafutie mema. (K)

INJILI: Mt 8:5-11
Yesu alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni.

TAFAKARI

IMANI KUBWA: Injili ya leo ipo kama kioo cha kujitazama. Inatukumbusha maneno tunayosema wakati wa misa kabla ya kukomunika. Ni maneno yaliyotoka kwa akida mmoja ambaye yawezekana hata hakuwa mcha Mungu sana. Akida huyu anatufundisha kuwa na imani kubwa isiyo na mashaka. Alimwamini Yesu na alitambua ana nguvu ipitayo nguvu za kawaida. Aliamini kwamba neno la Yesu lina nguvu ya uponyaji. Aliamini hivyo kutokana na kazi yake na mamlaka aliyokuwa nayo ya kutoa maagizo kwa waandamizi wake yakatekelezwa mara moja. Aliamini kuwa Yesu akitamka neno jambo la uponyaji litatendeka. Sisi tuliobatizwa katika kanuni ya Utatu Mtakatifu tunao ukaribu wa pekee sana na Yesu labda hata kumzidi huyu akida. Tutumie nafasi hiyo kumweleza Yesu yale yanayotusibu. Tuwe na imani kwa neno lake kwani neno lake linaponya na linaokoa. Mtu akiugua au akipata changamoto kubwa asikimbilie kwa waganga wa kienyeji bali akimbilie kwa Yesu. Akida huyu atufundishe pia unyenyekevu. Tukihudhuria misa kama hatustahili kumpokea Yesu, tusubiri tujitakase kwanza.

Sala: Ee Yesu mnyenyekevu, naomba uniongezee imani na unyenyekevu.