NOVEMBA 28, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 1 YA MAJILIO


Urujuani
Zaburi: Juma 1


SOMO 1: Yer 33:14-16
Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda. Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii. Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.

WIMBO WA KATIKATI Zab 25:4-5, 8-9, 10, 14.

 1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
  Unifundishe mapito yako,
  Uniongoze katika kweli yako,
  Na kunifundisha.
  (K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.
 2. Bwana yu mwema, mwenye adili,
  Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
  Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
  Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
 3. Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
  Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
  Siri ya Bwana iko kwao wamchao.
  Naye atawajulisha agano lake. (K)

SOMO 2: 1 Thes 3:12-13, 4:1-2
Ndugu zangu: Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote. Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa BwanaYesu.

SHANGILIO Zab 85:7
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana utuoneshe rehema zako, uwape wokovu wako.
Aleluya.

INJILI: Lk 21:25-28, 34-36
Siku ile kutakuwa ishara katika jua; na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi, mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia. Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu
BWANA NAKUINULIA NAFSI YANGU: Kipindi cha Majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Kipindi cha kwanza huanzia Dominika ya kwanza ya Majilio hadi tarehe 16 Desemba. Masomo ya kipindi hiki hutuelekeza juu ya ujio wa pili wa Bwana Yesu na hutualika kutubu wakati tukijiandaa kwa ujio wa pili wa Bwana wetu. Sehemu ya pili huanzia tarehe 17 hadi 24 Desemba. Kipindi hiki hutukumbusha juu ya ujio wa Yesu ulimwenguni kwa mara ya kwanza.

Katika Dominika yetu ya kwanza ya Majilio, tafakari ya neno la Bwana inaongozwa na zaburi ya wimbo wetu wa katikati, zaburi ya 25, “Ee Bwana nakuinulia nafsi yangu.” Hii ni zaburi ya mtu aliye katika upweke, aliyetengwa na marafiki wake wote. Hivyo anamkimbilia Mwenyezi Mungu kwa msaada. Anatambua kwamba kwa njia ya kusali, kujinyenyekeza na kuungama dhambi zake, ataipatia nafsi yake wokovu. Wataalamu wa Biblia wanatuambia kwamba zaburi hii ilimbwa na mfalme Daudi baada ya serikali yake kupinduliwa na Absalomu. Absalomu alikuwa mtoto wa Mfalme Daudi. Daudi alipinduliwa na kutelekezwa na marafiki wake kama Ahitofeli (2 Sam 15:12). Hivyo alimlilia Mungu kwa unyenyekevu na kuomba huruma na msaada (Zab 41:9; 55:12–14). Zaburi hii inatumika leo Dominika ya kwanza ya Majilio kuonesha kwamba nasi tutaokolewa kwa njia ya unyenyekevu na kumrudia Mungu. Haya ndio yatakayotusaidia kumwona Kristo pale atakapokuja tena kwetu kwa mara ya pili.

Katika somo la kwanza, tunakutana na unabii wa Yeremia juu ya wana wa Yuda. Unabii wa Yeremia unatolewa kipindi serikali ya Yuda ikiongozwa kama koloni la Babiloni chini ya mfalme Nebukadneza (2 Fal 24). Yuda ilikuwa koloni la mfalme Nebukadneza. Nebukadneza aliwataka Wayahudi kulipa kodi. Watu wa Yuda walitaka kujikomboa kwa kuomba msaada toka Misri. Nebukadneza aliposikia hili, alikasirika na kuwashambulia. Yuda ilikuwa chini ya kiongozi dhaifu aitwaye Zedekia. Nabii Yeremia anatoa unabii wa ujio wa kiongozi mpya. Atamchipushia Daudi shina litakalowakomboa watu wake na kuwafanya waishi kwa amani. Hili shina ni Yesu Kristo. Yesu ni tofauti na mfalme Zedekia. Yeye atawajali watu wake. Wenye njaa atawakumbuka siku zote.

Sisi tunapaswa kuwa Masiha na mkombozi kwa sehemu tunazoishi. Tuepuke kuwa dhaifu kama mfalme Zedekia. Tuwe tayari kuwajali walio na shida, tusikubali wadogo wanyanyasike au kuonewa. Kama ni baba wa familia, lazima tuoneshe ubaba wetu. Tusikubali familia zetu zinyanyaswe. Waajiri waoneshe pia utayari wa kuwajali wafanyakazi wao. Wasiwatelekeze na kuwafanya waishi katika shida. Ili tuweze kufanikisha haya, ni lazima tuwe jasiri, tupambane na woga na tuwe mstari wa mbele katika kuonesha utendaji kwa matendo. Tuwe tayari kupambana na woga na aibu. Woga utatufanya tushindwe kuwa watu wa haki, mwishowe utatufanya tukose mbingu.

Katika Injili, Bwana Yesu anatueleza kwamba kutakuwapo na siku ya mwisho na siku ya hukumu. Yesu anatutaka tuishi kihodari, ili siku ya mwisho isituangushe kama wasiokuwa na maarifa. Siku hiyo isitukute tukiwa tumetawaliwa na vionjo vyetu na anasa za kidunia. Lazima tuwe tayari kudhibiti vionjo vyetu. Tukiruhusu vitutawale, tutaishia kutekwa kirahisi. Hivyo yafaa tuangalie vilema vyetu na vionjo vyetu na kuvidhibiti leo. Tusiruhusu vionjo vya ulevi, uasherati na vinginevyo vitutawale. Tuwe na fadhila ya kiasi. Tuepuke kuruhusu sifa za ulimwenguni zitutawale. Pale tunaporuhusu tutawaliwe na sifa hakika tutashindwa kuwa wafuasi hodari wa Bwana, tutasahau pia mapungufu na dhambi zetu na mwisho tutapotoka kabisa
Yesu anasisitiza kwamba siku ya hukumu, mwezi na nyota zitatikiswa. Hii yamaanishwa kwamba wote walio maarufu katika ulimwengu huu, wenye kujiona kuwa na madaraka hakika watatikiswa. Huu ni mwaliko kwetu sisi. Tujifunze kunyenyekea hali tukiendelea na maisha yetu ya ufuasi hapa ulimwnguni. Mara nyingi tuna tabia ya kuwaiga wanamuziki hodari, wachezaji mpira na wasanii maarufu na kufuata maisha yao kana kwamba wao ni watu hodari wasiotikiswa. Sisi tunapaswa kumtumainia Mungu. Hawa ni wanadamu dhaifu, wasiokuwa na lolote jipya.

Sala: Ee Bwana, njoo, ufanye ulimwengu wetu kuwa sehemu yako ya amani na haki.