NOVEMBA 27, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 34 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Dan 7:15-27
Mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwulisa maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo. Wanyama hao wakubwa walio wannw ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele. Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali ya wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hadari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi, na mwingine ataondoka baada ya hao; haye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu. Naye atanena maneno kinyume chake aliye juu, naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakti. Akini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuyapoteza na kuyaangamiza, hata milele. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na mumtii.

WIMBO WA KATIKATI Dan. 3:82-87

 1. Wanadamu, mhimidini Bwana;
  Msifuni na kumwadhimisha milele.
  Bani Israeli, mhimidini Bwana;
  Msifuni na kumwadhimisha milele
  (K) Msifuni na kumwadhimisha milele.
 2. Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;
  Msifuni na kumwadhimisha milele.
  Watumishi wa Bwana mhimidini Bwana.
  Msifuni na kumwadhimisha milele. (K)
 3. Roho na nafsi zao wenye haki mhimidini Bwana;
  Msifuni na kumwadhimisha milele.
  Watakatifu na wanyenyekevu wa moyoni,
  mhimidini Bwana;
  Msifuni na kumwadhimisha milele. (K)

INJILI: Lk 21:34-36
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu
UMUHIMU WA KUKESHA: Tunaelekea mwisho wa mwaka wa Kanisa na tafakari yetu ni ya mambo ya mwisho. Neno hili linatutaka tusipoteze umakini katika kungojea ujio wa pili wa Masiha (parousia). Kuna hatari baadhi ya watu kuona ujio wa Masiha umechelewa na hivyo kupoteza umakini katika kujiandaa na hivyo kujiingiza katika mambo yasiyostahili. Tukumbuke Yesu alishatuambia ufalme wa Mungu utakuja ghafla bila kutegemea na bila taarifa rasmi. Tukeshe kwa kutenda matendo mema. Roho zetu ziwe na mafuta ya kutosha ili zisizimike. Tuwe na busara kama wale wanawali kumi waliochukua mafuta ya ziada kwa taa zao, hata bwana harusi alipokawia hawakutindikiwa. Sala, neno la Mungu, sakramenti mbalimbali, mafundisho tupatayo kutoka mamlaka funzi ya Kanisa na mahusiano mazuri na wanajamii ni baadhi ya nyenzo za kutusaidia kukesha ili ufalme usitukute kabla hatujajiandaa. Tahadhari alizotoa Yesu ni changamoto ambazo zinawaangusha wengi hata siku hizi. Hima, tupige vita ulevi na maangaiko ya ulimwengu huu.

Sala: Ee Yesu Mkombozi wangu, niepushe na malimwengu yanayonizonga.