AGOSTI 5, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 18 LA MWAKA

Kutabarukiwa Basilika la Mama Maria
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Hes 20:1-13
Wana wa Israeli, mkutano wote waliingia bara la Sini, katika mwezi wa kwanza; watu wakakaa Kadeshi; Mariamu akafa huko, akazikwa huko. Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni. Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana! Mbona mmewaleta Kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano,wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea. Bwana akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa, na wanyama wao pia. Bwana akamwambia Musa na Haruni, kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionesha kuwa mtakatifu kati yao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 95:1-2, 6-9

 1. Njoni, tumwimbie Bwana,
  Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
  Tuje mbele zake kwa shukrani
  Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
  (K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
  Msifanye migumu mioyo yenu.
 2. Kwa maana ndiye Mungu wetu,
  Na sisi tu watu wa malisho yake.
  Na kondoo za mkono wake,
  Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! (K)
 3. Msifanye migumu mioyo yenu,
  Kama vile huko Meriba,
  Kama siku ya Masa jangwani.
  Hapo waliponijaribu baba zenu,
  Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

INJILI: Mt 16:13-23
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni;na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu

TAFAKARI:
KUMKIRI KRISTO SIYO JAMBO RAHISI HIVI KAMA MTU HANA IMANI. Kwa maneno, mwonekano na hata matendo yetu ya nje twaweza kuonekana kuwa tunamkiri Kristo. Kumkiri Kristo huja kwa imani itokayo kwa Mungu mwenyewe anayeotesha imani kama mbegu hai inayokua taratibu na kukomaa. Petro anamkri Kristo kuwa ndiye Mwana wa Mungu aliye hai na hata anapewa mamlaka. Hapa Kristo anatangaza rasmi kuijenga jumuiya yake yaani Kanisa ambayo kwayo kazi yake ya wokovu wa ulimwengu itaendelezwa hata miisho ya dunia. Ni jumuiya ambayo msingi wake ni imara kiasi kwamba halitashindwa na nguvu za kuzimu. Kukosa imani kulimfanya Musa apige jiwe mara mbili na hivyo Mungu akamwadhibu kwa kutokuamini kwake. Musa alifia jangwani na hakupata kuigusa nchi ya ahadi.

SALA: Ee Bwana tunakuomba utujalie kukuamini na kukukiri wewe hasa mbele ya watu.