AGOSTI 4, 2021; JUMATANO: JUMA LA 18 LA MWAKA

Mt. Yohane Maria Vianney, Padre
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Hes 13:1-2, 25 – 14:1, 26:29, 34-35
Bwana alinena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kila kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anaka karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, ile nchi tuliyoipita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanayoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi. Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo. Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi; hao walioninung’unikia. Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu ndio miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu. Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko watakakokufa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 95:1-2, 6-9

  1. Njoni, tumwimbie Bwana,
    Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
    Tuje mbele zake kwa shukrani
    Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
    (K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
    Msifanye migumu mioyo yenu.
  2. Kwa maana ndiye Mungu wetu,
    Na sisi tu watu wa malisho yake.
    Na kondoo za mkono wake,
    Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! (K)
  3. Msifanye migumu mioyo yenu,
    Kama vile huko Meriba,
    Kama siku ya Masa jangwani.
    Hapo waliponijaribu baba zenu,
    Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

INJILI: Mt 15:21-28
Yesu aliondoka Genezareti akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha wototo na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

TAFAKARI:
IMANI HUPONYA: Pamoja na kwamba kulikuwa na ubaguzi kati ya Waisraeli na makabila mengine mama Mkananayo akiwa amejaa imani hakuona aibu kumkimbilia Yesu ili amponye mwanaye. Imani yake inadhihirika baada ya Yesu kumwambia kuwa chakula cha watoto hakiruhusiwi kutupiwa mbwa, lakini huyu mama alimjibu Yesu kuwa hata mbwa hula mezani kwa bwana zao. Tunajifunza wazi kuwa wokovu haukuja kwa ajili ya watu fulani tu bali ni kwa ajili ya watu wote walio tayari. Ndugu zangu, ubaguzi katika jamii yetu unatufanya tusiwasaidie wenzetu na hivyo kuwaacha wakiteseka na mizigo inayowaelemea. Yesu anamponya binti ya mama Mkananayo kwa njia ya imani ya mamaye. Tunaalikwa kumwamini Kristo aliye nguvu yetu na mganga wa roho zetu naye atatuponya na adhabu ya milele.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba imani thabiti ili tusitetereke katika maisha yetu.