AGOSTI 3, 2021; JUMANNE: JUMA LA 18 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Hes 12:1-13
Meriamu na Haruni walimnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Mariamu, na kuwaambia, tokeni nje ninyi watatu, mwend hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama pale mlamngoni pa hema, akawaita Haruni na Mariamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaamia, sikizeni basi maneno yangu; akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu Musa; yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; kwake kitanena mdomo kwa mdomo, maana, waziwazi wala si mafumbo; na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Mariamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Mariamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu, nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, usiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. Musa akamlingana Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:1-5,10-11

 1. Ee Mungu unirehemu, sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  (K)Ee Mungu uturehemu, kwa kuwa tumefanya dhambi.
 2. Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Unitakase dhambi zangu.
  Maana nimejua mimi makosa yangu,
  Na dhambi yangu i mbele yangu daima. (K)
 3. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo,
  Na kuwa safi utoapo hukumu.
  Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
  Mama yangu alinichukua mimba hatiani. (K)
 4. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

INJILI: Mt 14:22-36
Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena, akawaambia, Jipeni moyo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa hawawezi; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.

TAFAKARI:
IMANI NA MASHAKA YETU HUTUFANYA TUSIFANIKIWE KATIKA MAISHA. Petro anapata imani na kutembea juu ya maji lakini mashaka yanamfanya asifanikiwe kumfikia Kristo katika kutembea kwake juu ya maji. Aliondoa macho yake kutoka kwa Yesu akaogopa mawimbi. Sisi pia twaweza kuwa na mashaka juu ya mambo mengi yasiyo ya kawaida kwa ulimwengu huu, yanayotudai imani hai na thabiti. Tunapaswa kumwamini Kristo pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kama vile mawimbi ya bahari yalivyojitokea katika safari ya Petro. Changamoto hizi ziwe ni daraja ya kufikia malengo yetu na hivyo tusiziruhusu kabisa zitutatize katika kutembea. Tuwe na moyo wa kuzipokea kama vile Musa ambavyo hakusita kumsikiliza Bwana Mungu kwa sababu ya wivu wa Miriamu na Haruni juu yake. Tujifunze kwa Musa kwamba hata aliyetukosea tunayo sababu ya kumwombea.

SALA: Tunakuomba, Ee Yesu mwema, utujalie kuyakaza macho yetu kwako tujifunze kutoka kwako.