JULAI 29, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 17 LA MWAKA

Mt. Marta
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Kut 40:16-21, 34-38
Musa alifanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya. Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi, ile maskani ilisimamishwa. Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake. Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa. Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku; kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote, bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena. Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 84:2-5, 7, 10

 1. Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
  Naam, na kuzikondea,
  Moyo wangu na mwili wangu
  Vinamlilia Mungu aliye hai.
  (K)Maskani zako zapendeza kama nini,
  ee Bwana wa majeshi.
 2. Shomoro naye ameona nyumba,
  Na mbayuwayu amejipatia kiota,
  Alipoweka makinda yake,
  Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
  Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
 3. Heri wakaao nyumbani mwako,
  Wanakuhimidi daima.
  Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
  Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
  Huendelea toka nguvu hata nguvu,
  Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K)
 4. Hakika siku moja katika nyua zako
  Ni bora kuliko siku elfu.
  Ningependa kuwa bawabu
  Nyumbani mwa Mungu wangu. (K)

INJILI: Mt 13:47-53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea,watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

TAFAKARI:
MUNGU HANA UBAGUZI: Mungu amejaa upendo kwa wanadamu wote. Bwana wetu Yesu Kristo anaonesha hilo wazi kwamba ufalme wa mbinguni umefanana na juya (wavu wa kuvulia samaki) ambalo limetupwa baharini na kukusanya kila aina. Maana yake ni hii kwamba Mungu hambagui yeyote katika kumwandalia ufalme. Wale watakaokuwa tayari kubadilika na kuwa wema hao watatengwa na wale ambao hawakubadilika na hivyo kila mtu atawekwa panapomstahili. Lakini kwanza amewaacha wawe pamoja. Tunajifunza kuwa Kanisa ni jumuiya ya waamini wema kwa wabaya, na hivyo tujitahidi kusaidiana ili katika ule mwisho malaika watuchukue wote kuingia mbinguni. Tusibaguane katika jamii yetu tunamokaa, tuwe na huruma kwa wahitaji, tuwasaidie maskini ili wote tusafiri pamoja kuelekea mafanikio. Kama vile Mungu asivyobagua bado wema na wabaya, kwa nini sisi tubaguane kwa misingi ya rangi, udini, ukabila na ukanda? Tuachane na chuki, na tumwache Mungu aliye hakimu wa haki atuhukumu sisi sote kwa haki.

SALA: Wewe Mungu unatupenda bila kutubagua tunaomba utusaidie kuiga upendo huu katika mahusiano yetu na wenzetu.