JULAI 28, 2021; JUMATANO: JUMA LA 17 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Kut 34:29-35
Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema na Bwana. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawahusia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoa akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi uso wake Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 99:5-7, 9

 1. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
  Sujuduni penye kiti cha miguu yake, ndiye mtakatifu.
  (K)Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.
 2. Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake,
  Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake,
  Walipomwita Bwana aliwaitikia. (K)
 3. Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao.
  Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa. (K)
 4. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
  Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu,
  Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu. (K)

INJILI: Mt 13:44-46
Yesu aliwaambia makutano mifano, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.

TAFAKARI:
UCHAGUZI SAHIHI: Katika maisha yetu tunajikuta katika mazingira ya mkanganyiko wa mambo na vitu vingi hadi tunashindwa kufanya uchaguzi ulio sahihi. Injili leo inatupatia mfano wa watu wawili waliofanya uchaguzi sahihi baada ya kujua kuwa wanachoamua kina thamani kubwa kuliko walichonacho kwa sasa. Wa kwanza anauza alivyonavyo na kununua shamba lenye hazina iliyositirika. Wa pili ni mfanyabiashara, aliuza alivyokuwa navyo akanunua lulu moja tu yenye thamani. Kwa mfano wa hao watu wawili tunaalikwa kujifunza kuchagua kilicho cha thamani kubwa. Hazina yetu na lulu yetu ya thamani kubwa ni ufalme wa mbinguni. Ili kuipata ni lazima kuuza tulivyonavyo ili kuipata. Kuuza tulivyonavyo ni kuondokana kabisa na dhambi ili kukaribisha ufalme wa Mungu mioyoni mwetu ambao ni wa thamani kubwa kuliko maisha ya starehe ya dhambi.

SALA: Tunakuomba, Ee Mungu Mwenyezi, utujalie kutambua lulu na hazina ya ufalme wako ili tuitafute kwa nguvu zetu zote.