JULAI 26, 2021; JUMATATU: JUMA LA 17 LA MWAKA

Wat. Yoakimu na Anna, Wazazi wa Bikira Maria
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Kut 32:15-24, 30-34
Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, hiyo ni sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi. Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, hasira ya Bwana wangu isiwake; wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu. Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana, akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi; ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 106: 19-20. 21-22. 23

 1. Walifanya ndama huko Horebu,
  Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
  Wakaubadili utukufu wao
  Kuwa mfano wa ngombe mla majani.
  (K)Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
 2. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
  Aliyetenda makuu katika Misri.
  Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
  Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)
 3. Akasema ya kuwa atawaangamiza,
  Kama Musa, mteule wake asingalisimama,
  Mbele zake kama mahali palipobomoka,
  Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

INJILI: Mt 13:31-35
Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

TAFAKARI:
UFALME WA MUNGU HUANZA TARATIBU: Leo katika Injili tunafundishwa kwa mifano miwili, wa mbegu ya haradali na chachu. Ufalme wa Mungu, Yesu anaufananisha na mbegu ndogo kabisa ya haradali ambayo inamea na kuwa mmea mkubwa, maana yake ni kwamba neno la Mungu huanza taratibu na kukua kila siku na kuenea kwa watu wengi. Pia kwa mfano wa chachu (hamira) Yesu anaonesha jinsi ufalme wa Mungu unavyoenea. Kwa neno lake Kristo, ulimwengu mzima unapata kumtambua Mungu wa kweli. Jinsi ambavyo hamira kidogo huumua unga mwingi ndivyo neno la Kristo linaweza kubadilisha mienendo ya maisha yetu. Kwa njia hiyo lazima tutambue kuwa kazi yetu ya uinjilishaji inakuwa na mafanikio taratibu na hata kuwafikia watu wengi. Tujitahidi daima kuhakikisha kuwa maisha yetu yanaanza kama mbegu ya haradali au chachu na hata kutawanyika kwa watu wengine kwa mfano wa matendo na maneno yetu mema yenye kumtangaza Kristo.

SALA: Utupe neema yako, Ee Bwana, tusiache kutenda mema hata yakiwa ni madogo madogo.