JULAI 24, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 16 LA MWAKA

Sharbel Makhluf, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut 24:3-8
Musa aliwaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili za Israeli, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili akapeleka vijana na wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe.
Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15

 1. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
  Toka maawio ya jua hata machweo yake.
  Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
  Mungu amemulika.
  (K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
 2. Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
  Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
  Na mbingu zitatangaza haki yake,
  Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)
 3. Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;
  Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
  Ukaniite siku ya mateso;
  Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

INJILI: Mt 13:24-30
Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La, msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

TAFAKARI:
MUNGU NI MVUMILIVU: Kwa mfano wa shamba lenye mbegu njema na magugu tunajifunza uvumilivu wa Mungu kwa wanadamu wakengeufu wenye dhambi. Mkulima anawaambia wafanyakazi wake waache ngano ikue pamoja na magugu ili magugu yakikusanywa wakati wa mavuno yachomwe. Leo kupitia sehemu hii ya Injili tunajifunza kwamba Mungu hugawa mapaji yake kwa wote wachamungu na wadhambi kiasi kwamba wote hufaidi neema za Mungu. Kwa mfano mvua hunyesha katika shamba la mwenye haki na mdhambi, hii ni ishara kwamba Mungu anatuvumilia kama ambavyo mkulima anayavumilia magugu na hata kuyapalilia pamoja na mbegu njema na kuacha vikue vyote hata muda wa mavuno. Ukweli ni kwamba Mungu ametupatia muda wa kutafakari na kutubu, kugeuka toka magugu na kuwa ngano ili katika kuvunwa tuingie ghalani. Lakini watakaobaki kama magugu watachomwa moto. Siku ya hukumu ndivyo itakavyokuwa, wenye kustahili (ngano) watapewa makao mbinguni na wasiostahili (magugu) watachomwa moto. Tujitajidi kuwa mbegu njema ili wakati wa mavuno tuwekwe ghalani.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie kutubu na kurekebisha maisha yetu bila kujisahau hasa pale unapotuvumilia.