JULAI 22, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 16 LA MWAKA

Mt. Maria Magdalena
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut 19:1-2, 9-11, 16-20
Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo walifika jangwa la Sinai. Nao walipokuwa wameondoka Refilimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako kattika wingu zito, ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa; ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. Musa akawatoa watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za nchi za kile kilima. Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuru, mlima wote ukatelemka sana. Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.

WIMBO WA KATIKATI: Dan. 3:52-56

 1. Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu;
  Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
  Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
  Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
  (K)Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
 2. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
  Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)
 3. Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
  Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
 4. Umehimidiwa utazamaye vilindi,
  Uketiye juu ya makerubi;
  Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
 5. Umehimidiwa katika anga la mbinguni
  Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

INJILI: Mt 13:10-17
Wanafunzi walimwambia Yesu, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa masikio yao hawasikii vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.

TAFAKARI:
KUTUMIA VIPAWA VYETU: Kila mwanadamu amepewa kipaji chake ambacho humfanya awe alivyo. Kukitumia kwake na kutokitumia humfanya afanikiwe au asifanikiwe katika maisha. Katika Injili Yesu anatuambia mwenye nacho ataongezewa na siye nacho atanyang’anywa hata kidogo alichonacho. Kwa kutumia vipaji na karama zetu ndipo tunaweza kuyatambua mapenzi ya Mungu na kuyatenda. Tumepewa vipaji tuvitumie kwa faida yetu sisi na wenzetu. Kwa kuvitumia ipasvyo tutaongezewa yaani tutafaulu katika maisha na kwa kutotumia tutanyang’anywa kipaji hicho tulichopewa yaani hatuwezi kufaulu kamwe. Kwa kuyang’amua hayo kuwa tuko na nguvu ya kimungu ndani yetu tunaweza kutenda makubwa zaidi kwa manufaa ya jamii.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie neema ya kutambua vipaji vyetu na kuvitumia ipasavyo kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu hasa ya kiroho tukiutazamia wokovu.