JULAI 20, 2021; JUMANNE: JUMA LA 16 LA MWAKA

Mt. Apolinari, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut 14:21 – 15:1
Musa alinyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto. Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania kinyume cha Wamisri Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja. Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni makuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto. Ndivyo Bwana alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri. Ufuoni kwa bahari, wamekufa. Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya Bwana juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha Bwana, wakamwamini Bwana, na Musa mtumishi wake. Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

WIMBO WA KATIKATI: Kut. 15:8-10, 12, 17

 1. Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,
  Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu,
  Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
  Adui akasema nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara,
  Nafsi yangu itashibishwa na wao;
  Nitaufuta upanga wangu,
  Mkono wangu utawaangamiza.
  (K)Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.
 2. Ulinyosha mkono wako wa kuume,
  Nchi ikawameza.
  Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza;
  Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. (K)
 3. Utawaingiza, na kuwapanda
  Katika mlima wa urithi wako,
  Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae,
  Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana,
  Kwa mikono yako. (K)

INJILI: Mt 12:46-50
Yesu alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe. Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

TAFAKARI:
JAMAA WA KWELI: Bwana wetu Yesu Kristo alikuja kujenga jumuiya ya waamini wake hapa duniani ambayo haitakuwa na mipaka ya kikabila au ya kitaifa bali kuwafanya kuwa wamoja. Jumuiya hii itaongozwa na Kristo mwenyewe na kila mmoja katika jumuiya atakuwa jamaa yake wa kweli. Katika Injili tunasikia habari za ndugu zake wanaotaka kuzuia kazi yake ili waseme naye kwanza, naye anawaambia jamaa na ndugu zake ni wale wafanyao mapenzi ya Mungu. Sisi tu ndugu katika Kristo, jamaa moja ndani ya Kristo na kwa kuyatimiza mapenzi ya Mungu tunakuwa ndugu na jamaa halisi wa Kristo. Ipo misemo mingi sana katika jamii inayoonesha udugu wa kweli kati ya watu ukiondoa ule uhusiano wa damu. Mfano, “Akusaidiaye shidani ndiye rafiki” au “Undugu si kufanana bali kufaana.” Hii inaonesha kuwa urafiki unajengwa katika sababu maalumu, na hivyo ili kuwa ndugu, jamaa wa Kristo na Kanisa tunazo sababu ambazo ni imani katika Kristo na utendaji wa amri za Kristo aliye asili ya undugu wetu wa kweli. Tujitahidi daima kuwa ndugu zake Kristo kwa kulishika neno lake na kulitenda.

SALA: Bwana Yesu, tusaidie tujitahidi kulishika neno lako kwa mataendo yetu ili tuwe jamaa zako kweli.