JULAI 19, 2021; JUMATATU: JUMA LA 16 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut 14:5-18
Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandali gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Misri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi- hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. Wakamwambia Musa, Je! Lwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, tuache tuwatumikie Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, msiogope, simameni tu, mkaone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. Bwana akamwambia Musa, mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.

WIMBO WA KATIKATI: Kut. 15:1-6

 1. Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana;
  Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
  Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu;
  Naye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;
  Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
  (K)Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.
 2. Bwana ni mtu wa vita,
  Bwana ndilo jina lake.
  Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,
  Maakida yake wateule wamezama
  Katika bahari ya Shamu. (K)
 3. Vilindi vimewafunikiza,
  Walizama vilindini kama jiwe.
  Bwana, mkono wako wa kuume
  Umepata fahari ya uwezo,
  Bwana, mkono wako wa kuume wawasetaseta adui. (K)

INJILI: Mt 12:38-42
Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.

TAFAKARI:
KUTAFUTA ISHARA: Katika lugha ya Kiswahili kuna msemo usemao “Miluzi mingi humpoteza mbwa.” Miluzi hii inakuwa ni kelele tu kwa mbwa na mwisho hupotea asijue wapi alipoitwa na ni nani aliyemuita, na hata yawezekana akasikia hata mvumo wa upepo akadhani bwana wake amemwita. Tunazo kelele nyingi humu ulimwenguni za kisiasa, kichumi, kidini na kijamii. Hizi zote hutufanya tupotee njia na baada ya kupotea tunaanza kutafuta namna ya kuipata njia sahihi ili kurudi tulikotoka. Katika kuitafuta njia hii ya kurudia tulikotoka tunajikuta hasa kwa nyakati zetu hizi tukitafuta njia za mkato ya kutegemea muujiza ili kumwamini Mungu ambaye tunakuwa na tumaini kwake. Tumekuwa tukitafuta ishara kama Wayahudi ili kukomaza imani yetu na tumaini letu. Yesu anatufundisha kuwa ishara si kitu bila yeye azitoaye ishara hizo. Hivyo, kumtegemea Kristo aliyekufa na kufufuka ni bora zaidi kuliko kusubiri ishara ambazo tunadhani kuwa zitatufaa maishani.

SALA: Ee Yesu Kristo, tusaidie tukupende wewe kwanza bila kutafuta miujiza au ishara zako.