Mwaka B
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Yer 23: 1-6
Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! asema Bwana. Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana. Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka. Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana. Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili Bwana ni haki yetu.
WIMBO WA KATIKATI Zab 23 :1-6
- Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza,
Huniuhisha nafsi yangu.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. - Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake,
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako la fimbo yako vyanifariji. (K) - Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K) - Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SOMO 2: Efe 2: 13-18
Katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
SHANGILIO: Yn 15:15
Aleluya, aleluya,
Ninyi nimewaita rafiki,
Kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
INJILI: Mk 6: 30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.
TAFAKARI:
YESU ANAKUTAKA UWE MCHUNGAJI BORA: Katika Dominika hii, neno la Bwana linatoa onyo kali hasa kwa wale wachungaji waharibifu, wasiolichunga kundi lake inavyostahili. Sisi wabatizwa ni wachungaji kwa njia ya ubatizo wetu. Matendo yetu yanapaswa kuwatia wenzetu moyo. Sisi tuwe wachungaji wema na tulilishe kundi letu katika malisho salama. Huu ndio ujumbe mkuu tunaopaswa kutafakari leo.
Katika somo la kwanza, nabii Yeremia anawakemea wachungaji potofu. Hawa waliwatelekeza kondoo, na kuwaacha wakitangatanga na mwishowe kondoo kukaa katika mazingira hatarishi. Yeremia anatoa unabii toka kwa Mungu ambapo Mwenyezi Mungu anatangaza kulishughulikia kundi mwenyewe na kulipatia mchungaji atakayelilinda katika njia safi. Kondoo hawataishi mazingira hatarishi tena au kuonewa tena na adui. Ndugu zangu, unabii huu wa Yeremia uliwahusu wafalme wa Israeli na makuhani wake na viongozi wa dini. Wao waliwatelekeza wana wa taifa la Israeli. Walishindwa kuwalisha kwa mifano bora. Waliwaletea sanamu na tamaduni za mataifa maovu ili waziabudu (1Fal 11). Dhambi hizi ziliwafanya wana wa Israeli kukosa ulinzi wa Mungu, kutekwa na kupelekwa utumwani na mataifa ya kipagani. Yeremia anatumwa kuwakemea hawa viongozi kwani kwa mifano yao mibaya na kutokujali, kundi la Bwana linapata mateso makubwa. Mwenyezi Mungu anazidi kutoa matumaini kwa kusema kwamba atatafuta mchungaji mpya atakayeliongoza kundi kwenye njia sahihi zaidi. Unabii ulitimia kwa ujio wa Yesu.
Katika Injili, Yesu anajidhihirisha kuwa mchungaji imara tofauti kabisa na wale wa taifa la Israeli. Yesu anakuwa tayari kulionea huruma kundi lake. Yesu anawapeleka mahali pa faragha wanafunzi wake. Pia anakuwa tayari kuwahudumia makutano wanaokuja kwake. Yesu anawapenda kondoo wake na hataki watangetange kama kondoo wasio na mchungaji. Kama mchungaji, Yesu anawapatia kondoo wake chakula bora. Yesu anatupatia chakula bora na hataki siku zote tule jalalani. Yeye ametupatia Ekaristi Takatifu, chakula bora chenye nguvu za kutuvusha katika shimo la machafu na magumu ya ulimwengu huu.
Katika somo la kwanza na la Injili, twajifunza yafuatayo: kwanza tutambue kwamba Yesu ni mchungaji mwema na tuwe tayari kupokea yale aliyokwisha tuandalia. Tujue kwamba Ekaristi Takatifu ndiyo chakula chetu kama kondoo na neno la Mungu ndilo linalopaswa liwe taa yetu kama kondoo. Tujifunze kuvitumia vyakula hivi. Tuamini sakramenti zetu. Wakristo wengi wamepotoka kutokana na ushiriki mbovu wa sakramenti za Kanisa
Pili wachungaji wanapaswa kulilisha kundi lao chakula bora. Yafaa wachungaji tujiandae vyema, ili tuweze kuwafundisha kondoo wetu mafundisho na maarifa bora. Mafundisho ya mchungaji yaguse shida za kondoo wake na kuwatia moyo. Wale walio na huzuni watiwe moyo na tuepuke kuwakwaza kondoo wetu. Mchungaji ajitahidi kuwa na sifa njema machoni pa kondoo wake na jamii nzima. Hili litawatia moyo na kuwafanya kukua kiroho.
Katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu ametangaza kutafuta mchungaji mwingine. Hii ilitokea baada ya yule wa kwanza kushindwa. Sisi tutambue kwamba tukishindwa, Mungu atachagua wachungaji wengine lakini hili halileti picha nzuri. Sisi lazima tujitahidi tuwe wachungaji wa kutumainiwa. Tujitahidi na Mwenyezi Mungu atatusaidia.
Yesu amewapeleka wanafunzi wake leo sehemu ya faragha na kuwafanya watulie. Tendo hili litupatie fundisho hasa kwa baadhi yetu tulio na wafanyakazi. Tuwapatie wafanyakazi wetu muda wa faragha na mapumziko pia. Tuepuke kuwafanyiza kazi kama mashine. Wapatiwe muda wa kutulia pia. Wafanyakazi wenye mahitaji maalumu tuwe tayari kuwatimizia. Tuwapende wafanyakazi wetu kama watoto au ndugu zetu. Hili litatufanya tuishi kwa amani kama mtume Paulo anavyotueleza katika somo la pili.
SALA: Bwana ninakuomba nipate furaha katika kuyafanya mapenzi yako.