JULAI 17, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 15 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Kut 12:37-42
Wana wa Israeli walisafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. Na kundi kubwa la watu waliochangamana nao wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng’ombe, wanyama wengi sana. Nao wakaoka mikate isiyochachwa na ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula.
Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa Bwana, ambao wapasa kuangalia sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 136:1, 10-15, 23-24

 1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Yeye aliyewapiga Wamisri
  Kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Akawatoa Waisraeli katikati yao;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  (K) Fadhili zake ni za milele.
 2. Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Akawavusha Israeli katikati yake;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)
 3. Aliyetukumbuka katika unyonge wetu;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Akatuokoa na watesi wetu;
  Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)

INJILI: Mt 12:14-21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza.
Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.

TAFAKARI:
NIA MBAYA: Yesu alipokuwa akizidi kuponya wagonjwa watu wenye nia mbaya walipanga kumwangamiza. Nia yao ya kumwangamiza inatokana na ukweli kwamba yale aliyoyatenda yaliwachukiza sana na wakaona kuwa hawana tena la kujisifia mbele ya watu. Mafarisayo hawa walikuwa ni watu wa heshima kubwa na kwa mahubiri ya Yesu walionekana hawana nguvu tena hivyo wanapanga mipango ya kumwangamiza. Tunao Mafarisayo wa nyakati zetu, wao kazi yao ni kuhakikisha wenzao hawafanikiwi. Wanawaogopesha watu kwa miujiza hewa, wanawatangazia watu kiama na adhabu za kuogofya, wanahubiri matisho na hata kuhakikisha kuwa wanawaangusha wale wenye imani ya kweli. Hakuna haja ya kuwaogopa, bali tunapaswa kusimama imara na kuishi kadiri ya imani yetu thabiti nao watashindwa kututoa tulipo na kutuuzia nia zao mbaya.

SALA: Utujalie, Ee Mungu Mwenyezi, kuwawazia mema wenzetu na tuwe wepesi katika kufurahia mafanikio yao.