Bikira Maria wa Mlima Karmeli
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Kut 11:10-12:14
Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.
Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri,akawaambia, mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.
Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miino miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni Pasaka ya Bwana.
Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami natafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.
Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 116:12-13, 15-18
- Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kutangaza jina la Bwana.
(K) Nitakipokea kikombe cha wokovu,
na kulitangaza jina la Bwana. - Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Umevifungua vifungo vyangu. (K) - Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)
INJILI: Mt 12:1-8
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya Sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala, na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya Sabato.
Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya Sabato makuhani hekaluni huinajisi Sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.
TAFAKARI:
MILA NA DESTURI: Yapo mambo mengi ambayo hutufaidisha na kutujenga kimwili na kiroho katika jamii. Mambo haya yamejengwa hasa katika mila na desturi za watu mbalimbali kama familia, jumuiya, kabila na hata taifa. Kuna yale ambayo kimsingi hutujenga kweli na mengine hutufanya kuwa watumwa. Katika Injili leo tunasikia habari ya wanafunzi kuvunja masuke siku ya Sabato, siku ambayo kwa mila na desturi ilikuwa ni marufuku kufanya kazi. Kwa mila hii ya Sabato, wapo watu walioumia na kushindwa kuendelea kwa sababu hii na wengine wakabaki kuwanyanyasa wenzao kwa kujihesabia haki. Yesu anatufundisha kuwa yeye ni mkubwa kuliko Sabato, yaani yeye ni mkubwa kuliko mila na desturi zetu. Kuzivunja mila potofu zote hakututii hatia kama tunafuata ile njia ya kweli, kumfuata Kristo na amri zake.
SALA: Tunakuomba, Ee Mungu Mwenyezi, utusaidie tusikumbatie mambo yasiyotusaidia kukua kiroho.