JULAI 14, 2021; JUMATANO: JUMA LA 15 LA MWAKA

Mt. Kateri Tekakwitha, /Mt. Kamili wa Lellis, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Kut 3:1-6, 9-12
Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.
Bwana akasema: Tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.
Musa akamwambia Mungu, mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 103:1-4, 6-7

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee Nafsi yangu umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.
  (K) Bwana amejaa huruma na neema.
 2. Akusamehe maovu yako yote,
  Akuponya na magonjwa yako yote.
  Aukomboa uhai wako na kaburi,
  Akutia taji la fadhili na rehema. (K)
 3. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
  Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
  Alimjulisha Musa njia zake,
  Wana wa Israeli matendo yake. (K)

INJILI: Mt 11:25-27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

TAFAKARI:
UHUSIANO NA MUNGU: Wanadamu wenye kiburi hujivuna kujua kila kitu kiasi cha kujitukuza sana wenyewe. Uhusiano kati ya mwanadamu unahitaji unyenyekevu wa mwanadamu ili Mungu apate kumfunulia siri ya ufalme wake. Yesu anamshukuru Mungu kwa kuwaficha wenye hekima na akili (waliojaa kiburi) na kuwafunulia watoto wachanga kuhusu ufalme wa mbinguni. Kwa kawaida watoto wachanga huwa wanyenyekevu na husikiliza na kujifunza kutoka kwa wakubwa. Tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa wanyenyekevu kama watoto ili kwamba mbele za Mungu tuwe makini kusikiliza matakwa yake na kuyaishi. Mungu amejifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo ili kwamba watakaomwamini wapate kumwamini Mungu na wapate tuzo ya maisha ya furaha mbinguni.

SALA: Ee Mungu, tunaomba utufanye wanyeyekevu daima.