JULAI 12, 2021; JUMATATU: JUMA LA 15 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Kut 1:8-14, 22
Aliinuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua YusUfu Akawaambia watu wake, angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi, tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, kukitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.
Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 124

 1. Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
  Israeli na aseme sasa,
  Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
  Wanadamu walipotushambulia.
  Papo hapo wangalitumeza hai,
  Hasira yao ilipowaka juu yetu.
  (K)Msaada wetu u katika jina la Bwana.
 2. Papo hapo maji yangalitugharikisha,
  Mto ungalipita juu ya roho zetu.
  Papo hapo yangalitupita juu ya nafsi zetu
  Maji yafurikayo. (K)
 3. Na ahimidiwe Bwana;
  Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao.
  Nafsi yetu imeokoka kama ndege
  Katika mtego wa wawindaji,
  Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. (K)

INJILI: Mt 10:34-11:1
Yesu aliwafundisha mitume wake: Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga, kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.
Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.
Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

TAFAKARI:
UFUASI WA KRISTO NA MAFARAKANO: Kumfuasa Kristo ni jambo la hiyari wala siyo la lazima. Lakini mafarakano huja pale ambapo neno la Kristo linapochoma dhamiri zetu na kuzifunua wazi kuwa tu wakosefu. Kwa maisha yao mapya wafuasi wa Kristo wanakuwa kikwazo kwa wenzao katika familia. Mfano kama baba ameongoka, mama hajaongoka lazima kutatokea shida. Au kama watoto wameongoka na wazazi hawajaongoka lazima kuwapo misuguano ndani ya familia, wawili kwa watatu, watatu kwa wawili, baba na mwana na kadhalika. Ndugu zangu, nasi tunayo jamii tunayoishi nayo, sisi ni sehemu ya jamii hiyo. Nasi mara nyingi tunafarakana kwa sababu hatupendi kuambiwa ukweli juu ya hali zetu halisi. Na wale wanaotuambia tunawaona kuwa vikwazo na hata wakati mwingine tunawatupa kwenye shimo la matope kwa kuwapa majina kama, “Mnoko”, “Kichomi”, “Mwenye figisu”, “Mtakatifu,”, “Mlokole” na kadhalika. Haya yote ni kwa sababu ya neno la Kristo lenye kuyafunua maisha yetu na kutuambia kuwa tu wakosefu na tunapaswa kutubu. Kumbe, shida yetu hatutaki kutubu !

SALA: Ee Yesu Kristo, tunaomba utupe nguvu ya kukuchagua wewe bila kuhesabu gharama.