2021 JULAI 11 DOMINIKA: DOMINIKA YA 15 YA MWAKA

Mwaka B
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Amo 7: 12-15
Amazia alimwambia Amosi, Ewe mwona, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 85: 8-13

  1. Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
    Maana atawaambia watu wake amani,
    Hakika wokovu wake u katibu na wamchao,
    Utukufu ukae katika nchi yetu.
    (K) Ee Bwana utuoneshe rehema zako utupe wokovu wako.
  2. Fadhili na kweli zimekutana,
    Haki na amani zimebusiana.
    Kweli imechipuka katika nchi,
    Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
  3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
    Na nchi yetu itatoa mazao yake.
    Haki itakwenda mbele zake,
    Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

SOMO 2: Efe 1: 3-14
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, Habari Njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

SHANGILIO: Yn 1:12, 14
Aleluya, aleluya,
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.

INJILI: Mk 6: 7-13
Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

TAFAKARI:
JITOLEE KWA AJILI YA KAZI YA BWANA: Katika somo la kwanza, nabii Amosi haogopeshwi na vitisho vya kuhani Amazia. Kuhani huyu alikuwa kibaraka wa mfalme wa Israeli aliyeitwa Yeroboamu. Yeye alipokea pesa toka kwa mfalme ili aongee mazuri ya mfalme mbele ya watu. Mfalme alipokosea na kutenda dhambi, hakumuonya bali alimsifia. Yeye alitafuta tu kushibishwa na mfalme. Aliwahimiza watu waache kwenda kutolea sadaka hekaluni Yerusalemu na badala yake alijenga sanamu kubwa katika mji wa Samaria na hapa akawahimiza watu kwamba wasipande kwenda Yerusalemu kutolea sadaka. Alihimiza sadaka zitolewe kwa sanamu iliyoko Samaria (1Fal 12:31). Amazia alidiriki kuabudu sanamu ili apate pesa za mfalme.
Amosi alitumwa na Mungu ili kukemea uovu huu. Alimwambia mfalme aachane na uabudu sanamu, aache kuwakwaza na kuwapotosha watu. Akamwambia mfalme avunje vunje ile sanamu iliyoko Samaria na kuanza kwenda kuabudu Yerusalemu. Amazia aliposikia hili, alikasirika sana, aliona kwamba Amosi anataka kuharibu kazi yake. Hivyo alikasirika na kumwambia aondoke kabisa Samaria, aende Yerusalemu akatabiri huko na huko ndiko atakapopata riziki yake. Amosi anashangaa na kujibu kwamba yeye hakuja kutabiri kwa sababu ya pesa au maslahi binafsi. Yeye alikuwa mchunga kondoo na mtunza mikuyu, wala hakuzaliwa katika familia ya kinabii au kikuhani kumaanisha kwamba hakurithi kazi ya kinabii toka kwa ukoo wake. Yeye alichaguliwa na Mungu ili atoe unabii na hatafuti pesa yoyote au malipo, na yupo tayari kufa kwa ajili ya kazi yake.
Somo hili naomba litufundishe mambo matatu. Kwanza, kila mmoja anaalikwa kuwa kama Amosi leo yaani tujione kwamba utume wetu tumeupata toka kwa Bwana na hivyo tuupende utume wetu kama ilivyotokea kwa Amosi. Tunapoupenda utume wetu, tutakumbana na maadui lakini kwa nguvu ya Mungu, maadui hawa hawataweza kutushinda. Sisi tuepuke kushtushwa na maadui kama hawa. Pili, uaminifu kwa Mungu ulimtunza Amosi katika kazi yake ya kinabii. Ulimfanya apate nguvu ya kuwakemea watu mbalimbali. Nasi yafaa tutambue kwamba uaminifu utatupatia nguvu ya kusimama mbele za watu na kukemea mabaya. Tukikosa uaminifu tutakuwa na woga. Na woga utatufanya tuwe na aibu na kukosa nguvu ya kuuhubiri ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Tuwe waaminifu tupate kuifanya kazi ya Bwana. Tatu, tunapoingia katika utume, tusitafute maslahi binafsi kama ilivyofanya Amazia. Hapa tutaanguka. Kazi yoyote tutakayoifanya kwa ajili ya Bwana haitaacha kutupatia tuzo (1Kor 15:58). Tujitolee kwanza na Bwana atatulipa. Wengi wetu tumeshindwa kuiendeleza kazi ya Bwana kwa sababu ya kutanguliza tamaa ya maslahi mbele. Nne, kazi ya Bwana itatutetea. Tutakapoifanya kwa uaminifu, itatuokoa na anayetaka kutudhuru kama ilivyomuokoa Amosi, itatutetea kama ilivyotokea kwa Yeremia. Sisi tuwe na lengo moja katika utume wetu-lengo la kuipenda kazi ya Bwana. Hakika itatutetea katika unyonge wetu.
Injili yetu leo inatoka Marko 6: 7-13. Injili hii ni maelekezo ya Yesu kwa wafuasi wake ya namna wanavyopaswa kuenenda katika utume. Yesu anasema wayakung’ute mavumbi kwa wale watakaokataa kuwapokea. Wengi wetu huwa tunakung’uta mavumbi kwa haraka mno. Ukikanyagwa na mwenzako kidogo tayari umeshakung’uta mavumbi. Hii ni kufanya mchezo na agizo hili toka kwa Kristo. Tunapaswa kulibariki taifa la Mungu. Tusiwe wa kukung’uta mavumbi kwa haraka. Tusibakie katika kukung’uta mavumbi na kutoa maapizo. Hili litairudisha kazi ya Bwana nyuma.
Yesu aliwataka wafuasi wake wawafariji walio wadogo na wawatembelee wenye magonjwa. Mitume walipaswa kuepuka kushikamana na watu wa daraja fulani fulani au kikundi cha watu fulani fulani tu bali wawe rafiki kwa watu wote wa Bwana. Mtakatifu Fransisko wa Assisi alikuwa tayari kuambatana na wadogo na maskini. Nasi tufuate mwenendo huo huo toka kwa mtakatifu huyu.
Katika somo la pili mtume Paulo, anatoa shukrani kwa Mungu kwa kuwabariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo. Kwa njia ya Kristo, tunapokea baraka toka kwa Baba. Kwa damu yake, tunao ukombozi wetu na masamaha ya dhambi. Sisi tusiache kumkimbilia Kristo. Baba ametupenda katika Kristo wake. Tusiache siku zote kusali kwa kumpitia Kristo. Kristo ndiye uzima na uhai wetu. Ndani ya Kristo kunakaa utimilifu wote wa Umungu. Tumweleze Kristo shida zetu na hakika Baba atatusaidia.

SALA: Bwana Yesu, tufanye sisi tupate kuwa wajumbe wako wa kweli.