2021 JULAI 9 IJUMAA: JUMA LA 14 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mwa 46:1-7, 28-30
Israeli alisafiri pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka, kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua.
Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.
Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni: Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake, kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 37:3-4, 18-19, 27-28, 39-40

 1. Umtumaini Bwana ukatende mema,
  Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
  Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
  Naye atakupa haja za moyo wako.
  (K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.
 2. Bwana anazijua siku za wakamilifu,
  Na urithi wao utakuwa wa milele.
  Hawataaibika wakati wa ubaya,
  Na siku za njaa watashiba. (K)
 3. Jiepue na uovu, utende mema
  Na kukaa hata milele.
  Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
  Wala hawaachi watauwa wake. (K)
 4. Na wokovu wenye haki una Bwana,
  Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
  Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
  Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
  Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

INJILI: Mt 10:16-23
Yesu aliwaambia mitume wake: Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua
Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.
Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu

TAFAKARI:
KUVUMILIA MATESO: Yesu anatawahadharisha mitume wake juu ya mazingira wanayoenda kufanyia kazi ya uinjilishaji. Siyo hao tu, bali nasi katika mazingira ya leo tunajikuta katika mazingira yaleyale ambayo mitume walipewa tahadhari kwamba wanatumwa katika mazingira magumu. Tupo katika wakati wenye falsafa na mitazamo tofauti katika mambo ya imani na maadili ya jamii. Haya yote ni mazingira yanayokuwa mbwamwitu kwetu. Katika kazi ya uinjilishaji hatuna budi kuendelea mbele bila kurudi nyuma kwa sababu Kristo amekwishatuhakikishia kuwa mambo magumu yapo lakini tusiogope macho ya watu. Jambo lingine la kujifunza leo ni kwamba hatutendi kwa nguvu zetu bali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayetuongoza kusema yaliyo ya kimungu. Uvumilivu unahitajika katika kupambana na magumu haya hasa ya kutoka kwa ndugu na wajuani wetu wote ambao watakuwa na chuki juu yetu kwa sababu ya jina la Kristo. Tujitahidi kusoma alama za nyakati katika uinjilishaji wetu bila kumsahau Roho Mtakatifu atutiaye nguvu daima.

SALA: Utusaidie, Ee Bwana, kutambua kuwa kazi ya uinjilishaji ni ya Roho Mtakatifu na hivyo tuyasikilize maongozi yake.