JULAI 8, 2021 ALHAMISI: JUMA LA 14 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mwa 41:55-57; 42:5-7, 17-24
Nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.
Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kufudifudi mbele yake. Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema, tumetoka nchi ya kanaani ili tununue chakula.
Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi, ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, kweli, sisi tulimkosa ndugu yetu kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia; kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia , kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 33:1-2, 10-11, 18-19

 1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
  Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
  Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
  Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
  (K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi,
  kama vile tulivyokungoja Wewe.
 2. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
  Huyatangua makusudi ya watu.
  Shauri la Bwana lasimama milele,
  Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. (K)
 3. Tazama jicho la Bwana li kwa wamchao,
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

INJILI: Mt 10:1-7
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye;Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema.
Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

TAFAKARI:
UTUME: Mtume halisi wa Kristo anazo sifa zinazomtambulisha. Sifa hizo tunaziona katika Injili ya leo nazo ni hizi; kwanza lazima waitwe. Kabla ya kutumwa kila mmoja anayetumwa huitwa kwa jina lake. Yesu aliwaita mitume kumi na wawili na kuwatuma. Sifa ya pili ni kuitika na kukubali kutumwa. Sifa ya tatu ni kutumwa. Yeyote aliye wa Kristo lazima atumwe, siyo kujiamulia kwenda kutangaza Injili. Na sifa ya nne kati ya nyingi ni kwamba wanaotumwa wanapewa ujumbe. Yesu aliwapa ujumbe “Hubirini mkisema ufalme wa mbinguni umekaribia.” Mitume wanakuwa na sifa hizo na wanatekeleza maagizo ya mkubwa wao aliyewatuma. Ndugu Wakristo, sisi tumeitwa katika ubatizo na tumetumwa kuhubiri Injili kwa watu wote kila mmoja kwa nafasi yake kama alivyoitwa. Kuhubiri Injili kinyume na wito wako ni kujiita na kujituma.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie neema ya kutambua wito wako na tuwe tayari kuitika na kuhubiri yale utakayotutuma kuyahubiri.