Mt. Maria Goreti, Bikira na Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mwa 32:22-32
Yakobo aliondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo.
Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, sikuachi usiponibariki. Akamuuliza, jina lako ni nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema,niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.
Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 17:1-3, 6-8, 15
- Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Nikutazame uso wako katika haki. - Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku,
Umenihakikisha usione neno;
Nimenuia kinywa changu kisikose. (K) - Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K) - Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
Mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)
INJILI: Mt 9:32-39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.
Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.
Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.
TAFAKARI:
NGUVU YA KRISTO: Yesu anaendelea na kazi yake ya kuutangaza ufalme wa Mungu. Kwa nguvu yake ya kimungu anatoa pepo na mtu aliyepagawa na pepo huyo alimfunga ulimi asiweze kusema, anasema. Wayahudi walishangaa na kwa wivu Mafarisayo wakasema Yesu anatoa pepo kwa nguvu ya pepo. Lakini Yesu hakujihangaisha nao akazidi kufundisha na kuponya. Mwisho anaona huruma kwa watu waliohitaji mtu wa kuwaongoza. Hapa tunafundishwa kuwa tusikate tamaa daima katika kuhubiri Injili hasa kwa matendo yetu na tusichoke kusali kwa ajili ya kuwapata wachungaji wa kundi la Bwana ili waendeleze kazi ya kuhubiri. Tusali kwa ajili ya miito ya upadre ili tupate mapadre wa kuwalisha wanadamu chakula cha kiroho. Ni kwa nguvu ya Kristo tu haya yanawezekana, hivyo tuitegemee nguvu hiyo tusiwe na mashaka kama Mafarisayo.
SALA: Tunakuomba ee Mungu tuitegemee nguvu yako ili tuyashinde mashaka yetu.