JULAI 5, 2021; JUMATATU: JUMA LA 14 LA MWAKA

Mt. Antoni Maria Zakaria, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mwa 28:10-22
Yakobo alitoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto, na tazama, ngazi imesimamisha juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na Tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli, Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.
Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililosimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi

WIMBO WA KATKATI: Zab. 91:1-4, 14-15

 1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
  Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
  Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu
  na ngome yangu,
  Mungu wangu nitakayemtumaini.
  (K) Mungu wangu nitakayemtumaini.
 2. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
  Na katika tauni iharibuyo.
  Kwa manyoya yake atakufunika,
  Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;
  Uaminifu wake ni ngao na kigao. (K)
 3. Kwa kuwa amekaza kunipenda
  Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
  Kwa kuwa amenijua jina langu.
  Ataniita nami nitamwitikia;
  Nitakuwa pamoja naye taabuni,
  Nitamwokoa na kumtukuza. (K)

INJILI: Mt 9:18-26
Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake.
Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.
Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

TAFAKARI:
IMANI HUPONYA: Katika mazingira ya kawaida kabisa ya kibinadamu tunakumbwa na matatizo ambayo hata mengine hukosa majibu. Yapo magonjwa yanayotukatisha tamaa baada ya kukosa majibu ya matabibu na hata kufanya mwanadamu aone kuwa hastahili kuishi. Katika Injili tumesikia habari ya mama aliyetokwa damu miaka kumi na miwili. Alipatwa na kadhia ya kila aina na hata pengine alitengwa na jamii yake kwa kuwa alitokwa damu muda wote na hivyo kufanya hata asifanye kazi zake za kumsaidia mahitaji ya kila siku. Kwa imani kabisa kuwa Yesu atamsaidia akaona hata akienda kuongea naye bado watu watamsonga na hatapata muda wa mazungumzo, hivyo akabuni njia mbadala. Aliamua kwenda kugusa pindo la vazi la Yesu naye akapona. Imani kubwa sana yaweza kutuponya na kadhia za maisha yetu. Tumtegemee Kristo katika kupona matatizo yetu.

SALA: Tunaitumainia huruma yako, Ee Mungu, utujalie tukutafute bila kuchoka.