JULAI 4, 2021; DOMINIKA YA 14 YA MWAKA

Mwaka B
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Eze 2: 2-5
Bwana aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo. Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana Mungu asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 123

 1. Nimekuinulia macho yangu,
  Wewe uketiye mbinguni.
  Kama vile macho ya watumishi
  Kwa mkono wa Bwana zao.
  (K) Macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu. Hata atakapoturehemu.
 2. Kama macho ya mjakazi
  Kwa mkono wa bibi yake;
  Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.
  Hata atakapoturehemu. (K)
 3. Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
  Kwa maana tumeshiba dharau.
  Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
  Na dharau ya wenye kiburi. (K)

SOMO 2: 2 Kor 12: 7-10
Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili; mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

SHANGILIO: Yn 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

INJILI: Mk 6: 1-6
Yesu alitoka, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa Sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema Huyu ameyapata wapi haya? na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

TAFAKARI: WITO WA NABII:
Watakatifu wengi wamewahi kupitia mateso na changamoto mbali mbali kabla ya kupata ushindi na kuvishwa taji lao la utakatifu. Baadhi, walikataliwa kabisa na jamii na hata kuumizwa vibaya. Manabii wa Mungu, tangu Agano la Kale walikumbana na magumu ya namna hii. Hata Mwana wa Mungu, ambaye watu walimsubiri kwa muda mrefu sana, cha ajabu alipofika wengi walimpinga na hata watu wa nyumbani kwake hawakumuelewa (Yn 7:5). Hili tunaliona katika Injili yetu leo. Hili liliwafanya watu wa nyumbani mwake washindwe kufaidi miujiza yake. Sisi tusiige ukaidi wa watu kama hao. Tunapaswa kumpokea Yesu na kuyaheshimu maongozi yake na hakika tutamfaidi Yesu wetu zaidi. Huu ndio ujumbe tunaopaswa kutafakari leo.
Katika somo la kwanza, nabii Ezekieli anaonekana kuwa chombo cha Mungu cha amani. Alikuwa balozi wa Mungu kati ya watu wake Israeli kabla ya uvamizi wa jeshi la Babiloni huko Yerusalemu. Ukweli ni kwamba manabii walipewa nguvu ya Roho wa Mungu; nguvu ya kubainisha ukweli na haki na uaminifu katika mazingira yote ambayo sifa hizi zilifunikwa kwa uongo, ukosefu wa haki na wasiwasi. Katika kipindi cha nabii Ezekieli, hali ya kisiasa, kidini na maadili katika taifa la Yuda ilikuwa ya wasiwasi. Watu walikuwa wasumbufu kwa sababu hawakutaka kumsikiliza Mwenyezi Mungu (Eze 3:7). Katika hali hii, nabii asipojipa moyo, hakika atashindwa kutimiza kazi ya Bwana. Mwenyezi Mungu anamwambia Ezekieli, “Usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao” (Eze 2:6). Wanaweza wasiwasikilize maneno yako, lakini walau “watajua ya kuwa nabii amekuwapo miongoni mwao” (Eze 2:5). Huu ni wito wa nabii. Anapaswa kutangaza linalosemwa na Bwana bila kuogopa macho, maneno au dharau za watu.
Katika somo la pili, Paulo anaeleza upinzani aliokumbana nao kama mtume wa Kristo. Paulo aliyalinganisha matatizo mengi ya kichungaji yaliyolikabili Kanisa la Korintho kama mwiba katika nyama yake. Mwanzo aliomba kwamba mwiba huu utolewe kwake, lakini mwishowe alijifunza kuupokea mwiba huu. Alijifunza kuishi katika kejeli, mateso na magumu ambayo aliteseka nayo kwa ajili ya Kristo (2Kor 12:10). Sisi tumeitwa kuwa manabii na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunapaswa kujifunza kuwa na roho ya kunyenyekea na yenye kukubali magumu mbalimbali. Tusipokuwa watu wa kukubali kupokea magumu, hakika tutashindwa kufanikisha kazi ya Bwana.
Katika Injili, Yesu kama nabii anakumbana na vikwazo mbalimbali. Mwinjili Marko ameorodhesha matukio matano ambapo Yesu alikumbana nayo toka kwa viongozi wa Kiyahudi na ilimpasa ajitetee: kwanza ni kuhusu nguvu yake ya kusamehe dhambi (2:1-12); upendo wake kwa watoza ushuru na wadhambi (2:13-17); mitazamo yake juu ya kufunga (2:18-22); uelewa wake juu ya usafi wa utamaduni (2:23-28); na kuponya siku ya Sabato (3:1-6).
Lakini katika Injili ya leo, ni kusanyiko la watu wa nyumbani kwake ndio wanaompatia Yesu upinzani. Yesu anapitia kile walichokipitia Isaya, Yeremia na Ezekieli ya kuwa nabii hakubaliki nyumbani kwake. Ingawa watu wa Nazareti walifurahishwa sana na mafundisho yake na kukubali miujiza na matendo yake, walishindwa kwenda mbali zaidi. Badala yake, walianza kuchimba historia yake na umaskini wa familia aliyotoka. Waliruhusu mambo haya yawazuie kuwa na imani kwa Bwana Yesu na hivyo wanashindwa kupokea ujumbe wa wokovu toka kwa Yesu. Pengine nasi tunaweza kuwa kama watu wa Nazareti, tukawa tumejijengea fikra kwamba unabii wa kweli hauwezi kutoka sehemu fulani au tukashindwa kupokea ukweli kwa sababu tunadhani kwamba baadhi ya watu fulani hawezi kutuambia ukweli au chochote chenye kutujenga. Wapo baadhi wanaokataa kuwatii mapadre fulani fulani au kupokea sakramenti toka kwao kwa madai kwamba ni wenye umri mdogo au kwamba hawana Roho Mtakatifu. Hivyo tunadhania kwamba hawawezi kuwa na ujumbe au ujuzi wa kutuambia chochote. Yabidi tujichunguze nyendo zetu ili tusije tukamfukuza Yesu katika maisha yetu na kumzuia kutenda miujiza kati yetu na kwenda kwa wengine.
Sisi tunaiitwa kuwa manabii wa popote pale tunapoishi. Lazima tuwe tayari kusimama na kupinga matendo maovu ndani ya jamii, kuongea kwa ajili ya watu wasio na sauti na kuwatetea maskini na wanaonyanyaswa. Hatupaswi kurudishwa nyuma kutokana na matusi, kejeli au vitisho toka kwa wapinzani. Haya yote hayana budi kutupata. Lakini mwishowe nabii atapewa tuzo lake.

SALA: Bwana, niimarishe mimi katika utume wangu kama nabii nihubiri ujumbe wako.