JULAI 1, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 13 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mwa 22:1-19
Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu naye akasema, Mimi hapa. Akasema, umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako katika nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmoja wapo nitakaokuambia.
Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tunakwenda kule, tukaabudu na kuwarudia tena.
Basi Ibrahimu akazitwaa kuni na hiyo sadaka, akamtika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babaangu! Naye akasema, Mimi hapa mwanangu.akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi, wakaendelea wote wawili pamoja.
Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Mungu-yire, kama watu wasemavyo hata leo, katika mlima wa Bwana itapatikana.
Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utaumiliki mlango wa adui zako; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba. Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 116:1-6, 8-9

 1. Aleluya.
  Nampenda Bwana kwa kuwa anaisikiliza
  Sauti yangu na dua zangu.
  Kwa maana amenitegea sikio lake,
  Kwa hiyo nitamwita siku zote.
  (K) Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai.
 2. Kamba za mauti zilinizunguka,
  Shida za kuzimu zilinipita.
  Naliona taabu na huzuni;
  Nikaliitia jina la Bwana.
  Ee Bwana, nakuomba sana,
  Uniokoe nafsi yangu. (K)
 3. Bwana huwalinda wasio na hila;
  Naliadhilika, akaniokoa.
  Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako,
  Kwa kuwa Bwana amekutenda ukarimu. (K)
 4. Maana umeniponya nafsi yangu na mauti,
  Macho yangu na machozi,
  Na miguu yangu na kuanguka.
  Nitaenenda mbele za Bwana
  Katika nchi za walio hai. (K)

INJILI: Mt 9:1-8
Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu; umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.

TAFAKARI:
KUYASHINDA MAJARIBU: Kuwa na imani tu hakutoshi kama imani hiyo itakapojaribiwa haitasimama imara kujitetea. Ibrahimu anashinda mtihani toka kwa Mungu ambaye alimwita na akaitika wito wake. Imani thabiti aliyokuwa nayo kwa Mungu ndiyo ilimfanya asikate tamaa katika kukabili jambo gumu kabisa la kumchinja mwanaye wa pekee, Isaka. Mungu aweza kutupa mtihani ili kutuvusha katika hali yetu ya dhambi na kutuimarisha zaidi katika kuuelekea utakatifu. Tunapowaza na kuwazua ni nini tufanye, yaani kuwa na mashaka ndipo hapo tunaposhindwa kukabiliana na mitihani na kuikubali ili tuishinde. Ni kwa imani hiyo watu wanampelekea Yesu mtu aliyepooza wakijua wazi kuwa anazo nguvu za kumwokoa dhidi ya mapooza. Kwa imani yao Yesu aliwahurumia na kumponya mwenye kupooza. Imani ni tiba ya yasiyowezekana. Imani ni msingi wa mafanikio. Lakini imani hiyo lazima iwe katika matendo hai yasiyo kinyume na imani.

SALA: Ee Bwana tunakuomba utuongezee imani hasa tunapokumbwa na majaribu.