JUNI 30, 2021; JUMATANO: JUMA LA 13 LA MWAKA

Wat. Mashahidi wa Kwanza wa Kanisa la Roma
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mwa 21: 5, 8-20a
Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiliza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamkalaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabidhi, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, akamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 34: 7-8. 10-11. 12-13

 1. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote.
  Malaika wa Bwana hufanya kituo,
  Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
  (K)Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
 2. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake,
  Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
  Wana-simba hutindikiwa, huona njaa,
  Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu
  chochote kilicho chema. (K)
 3. Njoni, enyi wana, mnisikilize,
  Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
  Ni nani mtu Yule apendezwaye na uzima,
  Apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)

INJILI: Mt 8:28-34
Yesu alipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. Wale pepo wakamshihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote, na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.

TAFAKARI:
MUNGU ANATIMIZA AHADI ZAKE: Ilimlazimu Ibrahimu kusubiria miaka mia moja ili kuifikia ahadi ya Mungu kwake ya kuwa na mwana, mrithi wa uzawa wake mwenyewe. Muda mrefu ndiyo, lakini Mungu alikuwa na mpango mkamilifu kwa maisha ya Ibrahimu. Hata kama alifuata ushauri wa mkewe kupata urithi kwa mjakazi wake Hajiri, baada ya kupata mrithi kwa Sara, mkewe huyo huyo anamshauri Ibrahimu kumfukuza Hajiri na mwanawe. Mungu anatunza agano lake kwetu. Juhudi binafsi na suluhisho la haraka bila kumshirikisha Mungu havidumu. Maana Mungu anasikia sauti ya maskini aitapo. Yesu anatimiza ahadi yake aliposema, “Nimekuja ili wawe na uzima,” ama pia aliposema kuwa amekuja kuwatangazia wafungwa uhuru wao. Anawakomboa watu walioteswa na pepo waovu, ishara ya mwanadamu aliyetekwa na uovu, na ambaye Mungu kwa njia ya Yesu Kristo aliahidi kumuweka huru.

SALA: Ee Bwana utuweke huru kutokana na maovu yanayotuzunguka kuufikia ufalme wako wa watu huru.