JUNI 29, 2021; JUMANNE: JUMA LA 13 LA MWAKA

WAT. PETRO NA PAULO, MITUME
Sherehe
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Mdo 12:1-11
Herode mfalme alinyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa Kanisa Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohane, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo Kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa amelala katikati ya askari wawili amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika kule chumbani akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, jifunge, Kavae, viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, jivike nguo yako ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mikono ya Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 34:1-8

  1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
    Sifa zake kinywani mwangu daima.
    Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
    Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
    (K)Malaika wa Bwana awaokoa wamchao.
  2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
    Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
    Nalimtafuta Bwana akanijibu,
    Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
  3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
    Wala nyuso zao hazitaona haya.
    Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
    Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
  4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
    Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
    Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema,
    Heri mtu yule anayemtumainia Bwana. (K)

SOMO 2: 2 Tim 4:6-8, 17-18
Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya haya nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, Mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akinitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu u na yeye milele na milele.

INJILI: Mt. 16:13-19
Yesu alienda pande za Kaisaria Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

TAFAKARI:
NGUVU YA MSAMAHA: Watakatifu Petro na Paulo ni nguzo muhimu ya uanzilishi wa Kanisa la mwanzo na uinjilishaji. Wote wawili ni ishara ya nguvu ya Mungu inayombadilisha mwanadamu kupitia ukombozi na msamaha, na anavyokuwa muumini anayetambua neema za Mungu. Wote ni mfano wa nguvu ya msamaha wa Kristo. Huku Petro akiwa na historia ya kumkana Yesu mara tatu, Paulo alifahamika kuwa mtesi wa Kanisa kabla ya kuongoka. Baada ya kukutana na msamaha wa Yesu, ndipo wanapobadilika na kuwa kweli mitume shujaa wa Kristo, Petro kwa israeli taifa teule, na Paulo kwa mataifa mengine. Juhudi walizozionesha katika kazi ya uinjilishaji, hadi kuwa tayari kukumbana na kila aina ya changamoto katika utume wao, ilitokana na nguvu ya Roho wa Mungu na imani dhabiti waliokuwa nayo kwa Mungu.

SALA: Ee Bwana tunakuomba utujalie kuujua msamaha wako ulivyo, na tuwe mitume wako kweli kama Petro na Paulo.