JUNI 28, 2021; JUMATATU: JUMA LA 13 LA MWAKA

Mt. Ireneo, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mwa 18:16-33
Watu hao waliondoka uko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. Bwana akanena, Je, nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. Bwana akasema, kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; Lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha, usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? Bwana akasema, nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.
Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona huko arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, huenda wakaonekana humo thelathini? Akasema, Sitafanya nikiona humo thelathini. Akasema, tazama nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 103:1-4, 8-11

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.
  (K)Bwana amejaa huruma na neema.
 2. Akusamehe maovu yake yote,
  Akuponya magonjwa yako yote,
  Aukomboa uhai wako na kaburi,
  Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
 3. Bwana amejaa huruma na neema,
  Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
  Yeye hatateta sikuzote,
  Wala hatashika hasira yake milele. (K)
 4. Hatukutenda sawasawa na hatia zetu,
  Wala hatukulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
  Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
  Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)

INJILI: Mt 8:18-22
Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

TAFAKARI:
BWANA AMEJAA HURUMA: Ibrahimu anamsihi Mungu kwa ajili ya waadilifu walioishi kati ya watenda maovu wa Sodoma na Gomora. Kwa msisitizo Ibrahimu alimwomba Mungu kuwahurumia wachache walioonesha uaminifu. Kwa ajili ya watu hamsini, ama watu watano waadiifu, Bwana aliahidi kutowaangamiza waadilifu kati ya waovu. Mtu mmoja anapenda kumfuata Yesu, lakini anazuiwa na majukumu yake. Labda ni kwa ajili ya huyo mmoja aliyependa kumfuata kwenda kutangaza huruma ya Mungu watu wengi wangeokoka. Kristo anamwomba kuchukulia uinjilishaji kwa dharura kwani wakati umefika. Ulimwengu wetu unahitaji sana waumini wanaojitahidi kuishi kwa uadilifu, ambao kwa sala na ibada yao ulimwengu mzima utaokoka. Watu walio tayari kuyaacha yote na kumfuata Kristo kwa uaminifu bila kutazama nyuma. Jamii, taifa na familia zetu zinahitaji japo mtu mmoja kati yao aliye mwaminifu na kwa njia yake wengine watakombolewa.

SALA: Ee Mungu, nikufuate kwa uadilifu, ili kwa sala na ibada yangu, wanaonizunguka wapate kukombolewa.