JUNI 27, 2021; DOMINIKA YA 13 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Hek 1: 13-15; 2:23-24
Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yo yote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani; Maana haki yaishi milele. Yaani, Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 30: 1, 3-5, 10-12

  1. Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua,
    Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
    Umeniinua nafsi yangu,
    Ee Bwana kutoka kuzimu.
    Umeniuhisha na kunitoa
    Miongoni mwao washukao shimoni.
    (K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.
  2. Mwimbieni Bwana Zaburi,
    Enyi watauwa wake.
    Na kufanya shukrani.
    Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
    Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
    Katika radhi yake mna uhai.
    Huenda kuliko huja kukaa usiku,
    Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
  3. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
    Bwana uwe msaidizi wangu.
    Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
    Ee Bwana, Mungu wangu,
    Nitakushukuru milele. (K)

SOMO 2: 2 Kor 8 : 7, 9, 13-15
Kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote; na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.

SHANGILIO: Yn 1:12, 14
Aleluya, aleluya,
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.
Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.

INJILI: Mk 5: 21-43
Yesu alipokwisha kuvuka kurudi ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsongasonga. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.

TAFAKARI:
BWANA NI MWENYE UPENDO MKUU: Tafakari ya neno la Bwana katika Dominika ya leo inagusia juu ya uwapo wa shida na mateso ulimwenguni. Tunaelezwa kwamba chanzo chake si Mungu, bali ni chuki ya yule mwovu Shetani. Zaidi neno linaeleza kwamba mateso na kifo huzidi kutawala kwa yeyote yule anayeambatana na Shetani. Injili inatueleza kwamba Yesu ndiye mwenye kutuokoa kwenye vifungo vyote vya mateso na kifo na hivyo imani kwa Yesu ni jambo la msingi sana. Hii ndiyo yenye kuiletea dunia matumaini kama inavyotokea kwa mama anayetokwa na damu leo na afisa Jairo katika Injili leo. Lakini katika ulimwengu, baadhi ya matatizo yanabidi yatatuliwe na sisi wenyewe tusaidiane katika kuyatatua. Jambo hili tutalisikia kwenye somo la pili. Huu ndio ujumbe mkuu leo.
Katika somo la kwanza, mwandishi anaelezea juu ya lengo la Mungu kumuumba mwanadamu: ni ili apate nafasi ya kufurahi na Mungu milele. Kitabu hiki kimeandikwa kwenye miaka ya 180 K.K. huko Alexandria ambapo swali kubwa kipindi kile lilikuwa kwa nini tumeumbwa na kwa nini huku ulimwenguni kuna mateso? Wanafalsafa Waepikureo walisema hakuna Mungu na mateso waliyaona kama moja ya sehemu ya maisha, na hivyo mwanadamu ilimbidi apambane na kuhakikisha anayashinda. Hivyo, walipendekeza njia mbadala kama kujitenga na maskini ili tusipatwe na shida zaidi. Lakini mwandishi wa somo la kwanza anapingana na mtazamo huu. Yeye anasisitiza juu ya uwapo wa Mungu na anasema tena kwamba chanzo cha kilio na maumivu ulimwenguni ni yule mwovu Shetani. Mungu ni mwema kila wakati na kila alichoumba ni chema. Lakini Shetani sivyo. Yeye amekuwa mwenye wivu muda wote. Yeye ndiye aliyewadanganya wazazi wetu wa mwanzo kwa kuwadanganya waoneshe majivuno mbele ya Mungu ya kutaka kufanana na Mungu, wawe na ukuu kama yeye. Aliwafanya wawe watu wa tamaa, wasiridhike na kile walichopewa, watamani zaidi (Mwa 3). Yote haya yalisababishwa na wivu wa Shetani, kwa nini mwanadamu afaidi kiasi hiki? Kwa nini apendwe kiasi hiki? Kutokana na lile kosa, mengi tumeyapata. Hadi leo tumeangukia kwenye kifo, maumivu na magonjwa mbalimbali. Yamesababishwa na kosa moja la kutokutii. Katika somo hili, tunagundua kwamba Mwenyezi Mungu hafurahishwi na kilio au mateso yetu.
Sababu zilizomfanya Yesu kuja ulimwenguni ni kutusaidia kufuta kosa la wazazi wetu na kutufanya kuwa huru na kukifanya kifo kuwa daraja kwa maisha yajayo. Aliyafufua matumaini yaliyokuwa yamemezwa na Shetani. Hivyo, Yesu ndiye akipaye maana kifo chetu, atupaye matumani na kuona kwamba kifo chetu kinakuwa daraja la maisha ya baadaye. Yeye ni rafiki yetu na kaka yetu, Ni yeye tu aliye sababu ya matumaini kwetu na hili tunaliona kwenye Injili. Yeye anakuwa sababu ya furaha yetu. Yeye analionesha hili kwa kufanya miujiza miwili: kwanza, anamponya mama aliyekuwa mgonjwa kwa miaka 12. Ndani ya miaka hii, madaktari wa kibinadamu walishindwa kumtibu. Yesu anamuokoa leo. Yesu ana nguvu juu ya magonjwa yote, anaposhindwa mwanadamu, Yesu hashindwi. Tuwe na utayari wa kusimama na kumgusa Yesu kwa imani kama alivyofanya huyo mama. Tusiogope umati. Wengi wamemgusa Yesu kwa imani na amewaonesha miujiza maishani mwao.
Baada ya hili, Yesu anamfufua tena kijana wa ofisa mmoja. Lengo la kufanya hivi ni kumpatia kijana uhai na kuwafariji waombolezaji. Lengo la muujiza huu ni kuonesha kwamba yeye ana nguvu juu ya kifo na hivyo aliwataka wanadamu wamwamini; yeye ndiye atakayewapatia maisha ya umilele. Kwa anayemwamini Yesu, kifo huwa daraja la kuvukia kwenye maisha yajayo. Kama tulivyosikia katika somo la kwanza, kifo kililetwa na wivu toka kwa Shetani na kitazidi kutawala kwa wale wote wanaomtii Shetani. Hawa watapatwa na mauti ya milele. Lakini tunaomwamini Yesu, mauti ya pili haitatupata kamwe (Ufu 21:8).
Katika somo la pili, Paulo anawahimiza Wakristo wa Korintho kuwachangia Wakristo wenzao walioishi Yerusalemu. Hawa walikuwa kwenye dhiki kubwa kwani walikuwa wametengwa na Wayahudi wenzao kwa kitendo chao cha kuukubali Ukristo. Walinyanganywa ardhi, wakanyimwa ajira, na urithi toka kwa familia zao (1Pet 4:19). Jamii ya Wakristo ilibidi kukazana kuwasaidia ili wasinyanyasike. Sisi tunaalikwa kuiga roho hii ya kusaidiana. Tusikubali wenzetu wanyanyasike hasa wakati wa shida na matatizo.

SALA: Ee Yesu mwema, naomba unisaidie niwe na moyo wa kuwasaidia wenzangu na kuondokana na roho ya manyanyaso.