JUNI 26, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 12 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mwa 18:1-15
Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazana, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka langoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Ma yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu, wakasema, haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimi akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akamleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, hakika nitarudia wakati uu huu mwakani, na tazama, Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na Bwana wangu mzee? Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati uu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kuime. Akakana Sara, akisema, Sivyo, umecheka.

WIMBO WA KATIKATI: Lk 1: 46-50, 53-55

 1. Moyo wangu wamwadhimisha Bwana.
  Na roho yangu imemfurahia Mungu Mwokozi wangu.
  (K)Bwana alikumbuka rehema zake.
 2. Kwa kuwa ameutazama
  Unyonge wa mjakazi wake.
  Kwa maana, tazama, tokea sasa
  Vizazi vyote wataniita mbarikiwa. (K)
 3. Kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu,
  Na jina lake ni takatifu.
  Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi,
  Kwa hao wanaomcha. (K)
 4. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake:
  Ili kukumbuka rehema zake.
  Kama alivyowaambia baba zetu,
  Ibrahimu na uzao wake hata milele. (K)

INJILI: Mt 8:5-17
Yesu alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema,Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.

TAFAKARI:
SISTAHILI UINGIE KWANGU: Ibrahamu kwa utu wema, anawapokea wapita njia na kula nao, asijue kwamba anawapokea malaika. Wakamwachia Habari Njema kwamba mwaka unaofuata atapakata mzawa na mrithi wake. Ukarimu wake unakuwa ndio hitimisho la miaka mingi ya subira. Akida, mmoja naye anamwalika Kristo kwa imani kwamba atamponya bintiye, hata kama hakustahili kumpokea kwake. Kama usemavyo msemo, ‘Mgeni njoo mwenyeji apone,’ Yesu anaisifia imani ya akida na kufundisha kwamba wageni watajaliwa kula na uzao wa Ibrahimu katika karamu ya Bwana, huku taifa taule likibaki nje. Kumkaribisha Mungu na wajumbe wake katika maisha yetu kunabadili matatizo yanayotukumba na labda kupitia kwao tunafarijiwa. Kuwa wakarimu kwa wengine tunakuwa wakarimu kwetu wenyewe bila kufahamu. Mapendo ya Mungu ni kwa kila mtu, mgeni na mwenyeji.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie ukarimu na utu wema, ili nasi tuwahangaikie wasiojiweza.