MEI 31, 2021; JUMATATU: JUMA LA 9 LA MWAKA

BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Sef 3:14-18
Imba, Ee binti Sioni; piga kelele Ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, Ee Sioni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.

WIMBO WA KATIKATI: Isa. 12:2-6

 1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
  Nitatumaini wala sitaogopa;
  Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
  Naye amekuwa wokovu wangu.
  Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu
  (K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
 2. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
  Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
  Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
 3. Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
  Na yajulikane haya katika dunia yote.
  Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
  Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

INJILI: Lk 1:39-56
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti. Ikawa Elizabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, Kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

TAFAKARI:
UMEBARIKIWA KATIKA WANAWAKE: Utabiri kwamba Bikira angechukua mimba na angezaa mtoto ulifahamika kwa Waisraeli wote, na hivyo mabinti wengi walikuwa wanajitahidi kuishi vizuri ili waweze kupata upendeleo huo. Bikira Maria anapomtembelea Elizabeti, baada ya kupata nafasi ya kumzaa Kristo, anapaza sauti akisema, ‘Umebarikiwa kuliko wanawake wote’. Kumbe, bahati hiyo imeangukia kwa mama yetu Bikira Maria. Amekuwa ni mama pekee ambaye Mwenyezi amemteua ili awe mama wa mwanaye, Bwana wetu Yesu Kristo na hivyo anashiriki kwa njia moja ama nyingine katika ukombozi wa wanadamu Yeye ndiye atakayemchukua mimba, kumzaa, kumlea na kumnyonesha, na hivyo anakuwa tabernaculo na kwanza kumpokea Kristo. Elizabeti anapata ujumbe wa kuzaliwa kwa huyo mkombozi kupitia kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Bikira Maria ni mama wa Mkombozi. Anastahili heshima yake. Tuendelee kumheshimu mama yetu Bikira Maria. Zaidi sana tuendelee kumwomba mama yetu Bikira Maria aliye mshenga afikishe kwa mwanae sala na maombi yetu. Tunaye mama, mama yetu Maria, tunaye.

SALA: Ee Mungu, kwa maombezi ya Mama Bikira Maria tunakuomba upokee sala na maombi yetu wanao.