MEI 30, 2021; DOMINIKA: JUMAPIL YA 9 YA MWAKA

UTATU MTAKATIFU
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Kum 4:32-34, 39-40
Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya Mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lolote kama hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? je! watu wakati wowote wamesikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu? Kwa hiyo ujue, leo hivi ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 33:4-6, 9,18-20, 22

 1. Kwa kuwa neno la Bwana ni adili,
  Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
  Bwana huzipenda haki na hukumu,
  Nchi imejaa fadhili za Bwana.
  (K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
MaanaYeye alisema, ikawa;
Na Yeye aliamuru, ikasimama. (K)

 1. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
 2. Nafsi zenu zinamngoja Bwana,
  Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
  Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
  Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)

SOMO 2: Rum: 8:14-17
Kila mtu anaongozwa na Roho wa Mungu, Huyo ndiye mtoto wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena Roho ya utumwa iletayo hofu; Bali mlipokea Roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, aba, yaani, baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithi pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.

SHANGILIO: Ufu 1:8
Aleluya, aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.
Aleluya.

INJILI: Mt 28:16-20
Wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya, mpaaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza, kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

TAFAKARI:
TUNASAIDIWA NA IMANI YETU: Dominika ya Utatu Mtakatifu ni Dominika inayoadhimishwa baada ya Pentekoste. Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu mwenye kuwezesha yote. Katika kipindi cha Noeli, tuliushuhudia upendo mkuu wa Baba kumtuma mwanaye ulimwenguni. Katika fumbo la Paska, Mwana alikufa msalabani kwa ajili ya wanadamu wote. Roho Mtakatifu alilizindua Kanisa siku ya Pentekoste akalitia mafuta Kanisa na hivyo likazaliwa na kuanza utume wake. Katika Dominika yetu ya Utatu Mtakatifu, Kanisa linatutangazia kwamba yote hayo yaliyotendeka, hayakutendwa na miungu mitatu bali ni Mungu mmoja aliye katika Nafsi tatu zilizo sawa. Ndilo lengo la Kanisa Kipo kishawishi kikubwa cha kufikiria kwamba kuna Miungu mitatu kwa kufikiria kuna Mungu anayeumba, mwingine aliyekufa msalabani kutukomboa na mwingine aliyekuja kututakasa. Kanisa liliona hatari hii. Ndipo leo Kanisa linasisitiza kwamba yupo Mungu mmoja, mwenye kutenda yote. Basi, leo tumshangilie Mungu wetu, aliye mkuu kuliko yote.

Ukuu wa Mungu wetu unadhihirika kutokana na ukweli kwamba hakuna aliye sawa naye. Hakuna awezaye kuyafahamu mawazo yake wala njia zake kwa maana ni mkuu mno (Rum 11:33-34). Hata kile mwanadamu anachofahamu ni kwamba ni yeye mwenyewe ameamua kujifunua kwetu. Bila ufunuo, hakika hatutaweza kujua lolote kuhusu Mungu. Mungu anapojifunua kwetu, amejifunua katika Utatu. Hili siyo fundisho la kujitungia bali ni yeye mwenyewe aliamua kujifunua kwetu hivyo nasi yafaa tulipokee kama lilivyo. Tumezaliwa ulimwenguni na kuukuta ufunuo wa namna hii. Yafaa tulipokee fundisho hili kama lillivyo; huu ndio ukuu wa Mungu wetu.

Tatizo linakuja kwetu sisi katika kuelewa na kuelezea fumbo hili. Twaweza kujiuliza, mbona linapingana na sheria za kihesabu au mantiki ya mwanadamu? Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu na Roho Mtakatifu ni Mungu lakini si miungu mitatu bali ni Mungu mmoja. Je? mbona mantiki inakataa? Lakini tutambue mantiki ya mwanadamu tunayotumia ni ya kibinadamu na ni dhaifu na imebanwa na sheria za kidunia. Hii haiwezi kamwe kumtambua Mungu. Mungu ni zaidi ya mantiki tuliyonayo. Hatuwezi kuukataa Utatu Mtakatifu ati kwa sababu hauendani na mantiki au kanuni za mwanadamu; hapa ni kumkosea Mungu haki. Hii ni kwa sababu yeye aliyeumba mantiki tunataka abanwe nayo? Yeye ni juu ya mantiki ya mwanadamu

Na ukweli ni kwamba kwenye kulielewa hili fumbo, twahitaji imani. Hili fumbo ni kwa watu wenye imani. si kwa watu wasio na imani. Hili ni la muhimu. Mungu ni mkuu kuliko akili yetu. Hatuwezi kumfahamu Mungu bila ya yeye kuamua kujifunua kwetu.
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha maisha yote ya Mkristo. Mfano, kila tusalipo, hatuwezi kusali bila kutumia Utatu, tunapobatizwa na kuingizwa kanisani ni katika jina la Utatu (Mt 28:19), unapoomba baraka, ni kwa jina la Utatu. Hivyo, kama Wakristo, hatuwezi kufanya chochote bila Utatu kutumika.

Tunachoweza kukiona ndani ya fumbo la Utatu Mtakatifu ni upendo na tukikataa kuliamini ni kumkufuru Mwenyezi Mungu. Katika dini zote, Mungu hajajifunua kiupendo na kwa hali ya juu kabisa kama ilivyotokea kwetu sisi Wakristo. Kwetu Wakristo, Mwenyezi Mungu amejifunua katika hali ya juu kabisa Bwana Yesu ndiye aliyetufunulia fumbo la Utatu kwa undani zaidi. Alikuwa tayari kuutwaa mwili, na kuishi kati yetu na baadaye kumtuma Roho Mtakatifu ambaye ni kiongozi wa Kanisa zima. Tusikubali kutumia akili zetu na kuudhania vibaya upendo huu mkuu toka kwa Mwenyezi Mungu.

Hakuna aliye na ufahamu wa kumtambua Mungu kwa undani wote. Sote tunahitaji ufunuo wake. kila tukutanapo na fumbo hili, tuzidi kusali sana na kumwambia Mungu atusaidie tupate kumtambua na kumfahamu zaidi. Pia atusaidie kuondokana na majivuno ya bure ya kudhania kwamba kwa akili zetu tunaweza kumjua Mwenyezi Mungu bila kusaidiwa. Pia atusaidie kutambua nafasi ya mwanga wa Roho Mtakatifu katika kumjua Mungu.

SALA: Tunakuabudu kabisa kwa kupiga magoti na kusujudu mbele yako, ewe Utatu Mtakatifu. Ongoza akili zetu na mapendo yetu.