MEI 28, 2021; IJUMAA: JUMA LA 8 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 44: 1, 9-13
Haya na tuwasifu watu wa utauwa, Na baba zetu katika vizazi vyao. Baadhi yao hawana kumbukumbu, Wamepotea kana kwamba hawakuwako; Wamekuwa kana kwamba hawakuzaliwa, Wala watoto wao baada yao; Lakini hawa walikuwa watu wa utauwa, Wala kazi zao za haki hazisahauliki. Wema wao utawadumia wazao wao, Na urithi wao una wana wa wana; Wazao wao wanashikamana na agano, Na watoto wao kwa ajili yao. Kumbukumbu lao litadumu milele, Wala haki yao haifutiki kamwe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 149: 1b-2, 3-4, 5-6 , 9b

  1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya
    Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
    Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
    Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
    (K)Bwana awaridhia watu wake.
  2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
    Kwa matari na kinubi wamwimbie.
    Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
    Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
  3. Watauwa na waushangilie utukufu,
    Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
    Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
    Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. (K)

INJILI: Mk 11: 11-26
Yesu aliingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara. Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza na wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akisema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sabbu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akawaambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia,, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.

TAFAKARI:
MATUNDA YA KUISHI KWETU: Katika somo la kwanza tunaona babu yetu Yoshua ben Sira akiendelea kuwasifu watu waliopita ambao anawaita watu wa utauwa. Anawasifu kwa kazi zao nzuri na anasema licha ya kwamba wamepotea, yale waliyoyafanya hayatasahaulika. Wema walioufanya kuwahudumia wenzao utaendelea kubaki, na uzao wao utashikamana na agano, na anasema kwamba kumbukumbu lao litaendelea kudumu milele wala halitafutika kamwe. Ni kwa sababu walikuwa watu wema, waliishi ulimwenguni wakazaa matunda. Hawakaa bure, bali walikuwa wa faida, faida ambayo tunaiona vile vile katika Injili. Bwana wetu Yesu Kristo anaingia Bethania akiwa na njaa lakini anashindwa kupata matunda kutoka mtini. Basi, anauadhibu mti huo nao unakauka. Kristo anatufundisha kuwa na imani itakayotuwezesha kuendelea kuzaa matunda, na hayo matunda yawe ni matunda mema. Katika kuishi kwetu tujitahidi kufanya mambo mazuri kusudi tukikumbukwa tukumbukwe kwa uzuri. Kamwe tusijaribu kufanya watu watukumbuke kwa mabaya katika maisha yetu.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie kuwa watu wanaoishi kwa faida. Tuzae matunda, tuwe faida kwa wengine.