MEI 27, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 8 LA MWAKA

Augustini wa Canterbury, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 42:15-25
Sasa nitayanena matendo ya Bwana, nami nitayadhihirisha mambo yale niliyoyaona, kwa neno la Bwana vimekuwapo viumbe vyake, na kazi impendezayo ni sawasawa na amri yake. Jua litoapo nuru hudhihirika mahali pote; na kazi ya Bwana imejaa utukufu wake. Watakatifu wa Mungu hawawezi kuyatangaza maajabu na miujiza yake, walakini Mungu amewapa majeshi yake uwezo wa kusimama mbele ya utukufu wake. Yeye huchunguza vilindi, na moyo wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu, hutujulisha yaliyopita, na yatakayokuja, na kuzifunua alama za mambo yaliyofichwa. Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lo lote ambalo limefichwa naye. Matendo makuu ya hekima yake ameyaratibisha, ambaye, Yeye ni mmoja tu, tangu milele na hata milele; hakuzidishiwa kitu, wala kupunguziwa kitu; wala yeye hana haja ye yote ya mshauri. Ee ajabu ya uzuri wa viumbe vyake!mtu angeweza kuliona hilo hata kwa habari ya cheche. Vitu vyote vyaishi na kudumu daima, na kwa kila haja vyote vyamtii. Vyote vinahitilafiana, wala hakufanya cho chote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio; naye ni nani atakayekinai kwa kuutazama utukufu wake?

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 33:2-9

  1. Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
    Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
    Mwimbieni wimbo mpya,
    Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
    (K)Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika.
  2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
    Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
    Huzipenda haki na hukumu,
    Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
  3. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika,
    Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
    Hukusanya maji ya bahari chungu chungu,
    Huviweka vilindi katika ghala. (K)
  4. Nchi yote na imwogope Bwana,
    Wote wakaao duniani na wamche.
    Maana Yeye alisema, ikawa;
    Na Yeye aliamuru, ikasimama. (K)

INJILI: Mk 10:46-52
Walifika Yeriko; Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

TAFAKARI:
WATAKA YESU AKUFANYIE NINI? Leo katika Injili tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo akifika Yeriko, na akiwa njiani anakutana na Bartimayo mwana wa Timayo, ambaye alikuwa kipofu mwombaji. Alikuwa anaketi kando ya njia kwa ajili ya kuomba msaada. Lakini kipofu huyu alikuwa kipofu wa mwili tu ila alikuwa anaona kiimani, ndipo aliposikia kwamba Yesu wa Nazareti anapita basi akapiga kelele akimwomba mwana wa Daudi amrehemu. Hakukoma kupiga kelele licha ya watu waliojaribu kumzuia, ndipo Yesu alipozisikia hizo kelele na jitihada zake na kumwita. Akamuuliza anataka amfanyie nini? Naye bila ya kupepesa macho alijibu anataka kuona. Na mara kipofu yule alipata kuona. Yesu daima anakaa mbele yetu tunapokuwa tunaabudu Ekaristi Takatifu, tunapokuwa mbele yake yasomwapo Maandiko Matakatifu katika adhimisho takatifu na tunapokuwa mbele ya watumishi wa Mungu. Daima Yesu yupo katikati yetu na anatuuliza kila siku, “Wataka nikufanyie nini?” Sisi tupeleke maombi yetu bila kusita kwa Kristo, kwa imani, na tusitie mashaka, Kristo atatutimizia.

SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, ufungue macho yetu kwa imani dhabiti ili daima tukuone unapokuwa pamoja nasi.