MEI 26, 2021; JUMATANO: JUMA LA 8 LA MWAKA

Filipo wa Neri, Padre
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 36:1, 4-5, 10-17
Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe; uangalie, uwatishe mataifa yote; uuinue mkono wako juu ya watu wageni. Wakujue wewe kama sisi tukujuavyo, ya kwamba hakuna Mungu ila Wewe peke yako. Tuoneshe ishara tena, na kufanya mambo ya ajabu; uutukuze mkono wako, naam, mkono wako wa kuume. Uwakusanye kabila zote za Yakobo, na kuwafanya urithi wako kama siku za kale. Ee Bwana, uwarehemu watu walioitwa kwa jina lako, na Israeli uliyemwita mzaliwa wa kwanza wako. Uuonee huruma mji wa patakatifu pako, Yerusalemu, mahali pako pa raha; uujaze Sioni adhama yako, na patakatifu pako utukufu wako. Uwashuhudie wale waliokuwa viumbe vyako tangu awali, na kuyathibitisha maneno ya unabii yaliyonenwa kwa jina lako. Uwajazi wakungojao, na watu watasadiki manabii wako. Ee Bwana, uisikilize sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako; na wote wakaao duniani watajua ya kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 79:8-9, 11, 13

 1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu
  Rehema zako zije kutulaki hima.
  Kwa maana tumedhilika sana.
  (K)Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe.
 2. Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
  Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
  Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
  Kwa ajili ya jina lako. (K)
 3. Na sisi tulio watu wako,
  Na kondoo za malisho yako,
  Tutakushukuru milele;
  Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

INJILI: Mk 10:32-45
Walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia; wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata, akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka. Na Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

TAFAKARI:
KUTUMIKA SIYO KUTUMIKIWA: Kila mmoja wetu anapenda kuwa mkubwa. Anapenda kuwa na madaraka. Shida iliyopo ni kuwa hatufahamu hasa kwa nini tuwe wakubwa, kwa nini tuwe na madaraka. Wengine hudhani kwamba madaraka ni kwa ajili ya kupata sifa, kusifiwa na watu, au kwa ajili ya kunufaika na marupurupu anayopata kwa madaraka hayo. Kristo leo anatufundisha maana halisi ya kuwa mkubwa. Ukubwa ni kutumikia na siyo kutumikiwa. Ndiyo maana wana wa Zebedayo wanapoomba mmoja kuketi mkono wa kushoto na mwingine kuketi mkono wa kuume katika ufalme wa Yesu, yeye anawaambia kuwa hawajui wanaloliomba. Kristo hataketi mkono wa kuume wa Mungu kwa sababu ya ukubwa tu, bali hasa kwa ajili utumishi, utumishi ambao mwenyewe yupo tayari hata kumwaga damu yake, kwa ajili yake. Ndiyo maana anawaambia kama wapo tayari kukinywea kikombe atakachokinywea, au ubatizo atakaobatizwa yeye. Wao wanajibu kijuujuu tu kwamba wapo tayari. Kwa kweli ubatizo na hicho kikombe watakinywea kwa namna ambavyo watapambana kutetea imani yao. Watupata ukubwa kwa utumishi.

SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, utufundishe maana halisi ya kuwa viongozi, yaamo kutumikia na siyo kutumikia.