MEI 25, 2021; JUMANNE: JUMA LA 8 LA MWAKA

Mt. Beda, Mhashamu, Padre na Mwalimu wa Kanisa/ Mt. Gregori VII Baba Mt/ Mt. Maria Magdalena wa Pazi, Bikira
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 35:1-12
Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuzingatia amri ndiye aitoaye kafara ya amani; amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora; naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabihu ya kushukuru. Kuuacha uovu kwampendeza Bwana, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho. Lakini ujihadhari usitokee mbele za Bwana mikono mitupu; maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri. Toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu tamu yake yafika mbele zake Aliye juu. Dhabihu ya mwenye haki yakubalikana, wala kumbukumbu lake halisahauliki. Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uoneshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe; na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu. Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba. Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 50:5-8, 14, 23.

 1. Nikusanyie wacha Mungu wangu
  Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
  Na mbingu zitatangaza haki yake,
  Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
  (K)Nitamwonyesha wokovu wa Mungu
  autengenezaye mwenendo wake.
 2. Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena,
  Mimi nitakushuhudia, Israeli;
  Mimi ndimi niliye Mungu, Mungu wako.
  Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele zangu daima. (K)
 3. Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru,
  Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
  Atoaye dhabihu za kushukuru,
  Ndiye anayenitukuza.
  Naye autengenezaye mwenendo wako,
  Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)

INJILI: Mk 10:28-31
Petro alimwambia Yesu, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza.

TAFAKARI:
UKARIMU KWA MUNGU: Leo tunafundishwa kuwa wakarimu kwa vile Mungu mwenyewe ni mkarimu. Jana tuliona jinsi tajiri alivyokosa ukarimu na kuamua kuondoka kwa huzuni. Petro anamuuliza Bwana, wao wameacha vyote wakamfuata, je, watapata nini? Ndipo Kristo anamwambia kwamba hakuna mtu aliyeacha vitu vyote kwa ajili ya Injili na kwa ajili yake akapoteza, ila atapata mara mia wakati huu na wakati ujao atapata uzima wa milele. Huo ndio ukarimu wa Mungu. Tunapotoa kwa ajili ya Mungu, hatupotezi, tunajiwekea hazina mbinguni. Msisitizo huu unaendelea katika somo la kwanza. Tunaambiwa kwamba yeye anayetoa sadaka kwa maskini basi anatoa dhabihu ya kushukuru. Mwenyezi Mungu anataka tusiwe watu wachoyo anasema tusitokee mbele za Bwana mikono mitupu, tutokee na kitu kwa ajili ya Mungu. Tumpe Mungu kwa ukarimu kwa sababu yeye ndiye aliyeanza kutupatia sisi. Bila yeye tusingekuwa na kitu. Bwana si mchoyo, yeye anatulipa. Tena tunaambiwa anatulipa mara saba. Mungu wetu ni mkarimu, nasi tuwe wakarimu.

Sala: Ee Bwana Yesu, uliye mkarimu, utujalie moyo wa ukarimu, kutoa kwa ajili ya Injili na tuwasaidie wengine wanaohitaji msaada.