MEI 24, 2021; JUMATATU: JUMA LA 8 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: YbS 17:24-29
Bwana Mungu huwajalia wale watubuo kurudi, na wao wanaopotewa na subira kuwafariji. Basi umrudie Bwana na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo; umgeukie tena Yeye Aliye juu, ayageue maovu, uyakirihi yaliyo machukizo. Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani. Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi Bwana, Ee ajabu ya wingi wa rehema za Bwana, na ya masamaha yake kwao wanaomgeukia!

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 32:1-2, 5-7

 1. Heri aliyesamehewa dhambi,
  Na kusitiriwa makosa yake.
  Heri Bwana asiyemhesabia upotovu.
  Ambaye rohoni mwake hamna hila.
  (K)Mfurahieni Bwana, shangilieni, enyi wenye haki.
 2. Nalikujulisha dhambi yangu,
  Wala sikuuficha upotovu wangu.
  Nalisema, nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
  Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
 3. Kwa hiyo kila mtu mtauwa
  Akuombe wakati unapopatikana.
  Hakika maji makuu yafurikapo,
  Hayatamfikia yeye.
  Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
  Utanizungusha nyimbo za wokovu. (K)

INJILI: Mk 10:17-27
Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda ukauze ulivyo navyo vyote. Uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.

TAFAKARI:
NIFANYE NINI KUURITHI UZIMA WA MILELE? Katika Injili ya leo tunamwona mtu mmoja ambaye anatambulika kama tajiri kijana akimfuata Yesu na kumuuliza nini afanye ili kuurithi uzima wa milele. Na Kristo anatoa mambo ya kufanyika. Cha kwanza ni kushika amri, mtihani ambao kijana huyo anashinda pale anaposema amezishika tangu ujana wake. Cha pili anamwambia, auze vyote alivyonavyo awape maskini, kisha amfuate Kristo. Tunaambiwa kwamba huyu ndugu alikuwa na mali nyingi na hivyo aliamua kuondoka zake kwa huzuni kwa vile hakuwa tayari kuuza mali alizokuwa amehangaikia kuzipata. Katika maisha yetu kunaweza tukawa na vitu ambavyo vinatunyima nafasi ya kuingia mbinguni. Uzima wa milele ni bora kuliko dhambi zetu. Katika somo la kwanza Yoshua ben Sira anadhihirisha wazi kabisa kwamba Mungu hapati faida yoyote kwa wale wote ambao wanapotea, ila anapata kwa wale wanaoishi na kumtolea Mungu shukrani. Hivyo, ili tuwe hai yatupasa kupambana ya yote yanayotutenga na Mungu hasa dhambi zetu tunazozitenda kwa kuzipenda sana ambazo mwishowe hutuletea vilema vya kiroho.

SALA: Ee Mungu Baba yetu, utusaidie kupambana na vilema vyetu, tupambane na dhambi zetu ili tuweze kukidhi vigezo vya kurithi uzima wa milele.