MEI 23, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA PENTEKOSTE

Sherehe
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Mdo 2:1-11
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana,
Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao Wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 104:1, 24, 29-31, 34

 1. Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
  Wewe, Bwana, Mungu wangu,
  Umejifanya mkuu sana;
  Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
  Dunia imejaa mali zako.
  (K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
 2. Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
  Na kuyarudia mavumbi yao,
  Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
  Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)
 3. Utukufu wa Bwana na udumu milele;
  Bwana na uyafurahie matendo yake.
  Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
  Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

SOMO 2: 1 Kor 12:3b-7, 12-13
Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

SHANGILIO
Aleluya,aleluya,
Uje Roho Mtakatifu,uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.

INJILI: Yn 20:19-23
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

TAFAKARI:
NJOO ROHO MTAKATIFU: Katika sherehe hii, tunaadhimisha namna Roho Mtakatifu alivyolishukia kundi dogo la Wakristo (waamini 120, Mdo 1:15) ambalo lilikuja kuwa chembe ya upandikizaji na ueneaji wa Kanisa; taifa takatifu la Mungu. Roho Mtakatifu alilizindua Kanisa siku ya Sikukuu ya Pentekoste ya Kiyahudi akaanzisha taifa jipya la Mungu lenye watu kutoka katika kila kabila, lugha na rangi likiunganishwa na imani moja katika Kristo. Roho Mtakatifu ndiye mwenye kuleta umoja kwa jamii hii na kuwafanya wote wasafiri pamoja kama taifa takatifu la Mungu.

Zaburi ya wimbo wa katikati leo ni Zaburi ya 104: “Waipeleka Roho yako Ee Bwana, nawe waufanya upya, upya uso wa nchi.” Hii ni zaburi iliyoandikwa baada ya mwandishi kutafakari tukio la gharika kuu, jinsi ulimwengu ulivyoangamia, jinsi watu maarufu na mali zao zilivyoangamia vibaya (Mwa 6). Lakini baada ya muda, ulimwengu ukajaa tena watu. Mwandishi anapoyatafakari haya, anashangaa na kusema “Mungu akitoa roho yake ulimwenguni, hakika ulimwengu unaangamia na kuoza. Lakini pale arudishapo roho yake juu ya uso wa nchi, ulimwengu unapata tena uhai.”
Huu ndio ukuu wa Roho wa Bwana. Ndiye mwenye kuleta uhai. Tumwalike akae kwetu kwani yeye ndiye uhai wetu. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, kabla roho ya Bwana kukaa juu ya uso wa nchi, dunia ilikuwa giza na utupu. Roho ya Bwana ilipotua juu ya uso wa nchi, dunia ilipata nuru na uhai (Mwa 1:2-5).
Watu wa enzi za Nuhu na wale wa Sodoma waliifukuza roho ya Bwana toka katika miji na vijiji vyao; kilichowapata ni kifo; waliokuwa wanajenga mnara wa Babeli waliitupa tena huyu roho pembeni, yaani lugha zao zikachanganywa (Mwa 11:1-9). Wakashindwa kujenga chochote. Sisi tusimfukuze Roho wa Bwana kati yetu. Roho ya Bwana ilikosekana katika ulimwengu, vitu vya ulimwengu vitakosa uhai, vyaweza hata kutugeuka na kuwa sumu kwetu. Lakini wakati ule watu hawakuelewa vizuri nini roho ya Bwana. Sisi tunaelewa vyema ni Roho Mtakatifu, Nafsi ya tatu ya Mungu.

Katika Injili yetu ya leo, tunamkuta Yesu akiongea na kundi dogo la watu kumi na moja jioni ya siku ya ufufuko wake. Kundi hili lipo katika hofu na masikitiko na kukata tamaa:Yesu anatokea mbele yao na kulipatia amani. Anawavuvia Roho Mtakatifu kama ishara ya kuwapa uhai mpya na analipatia madaraka ya kusamehe dhambi. Aliendelea kujitokeza kwa kundi hili na kabla ya kupaa kwake, aliliagiza lisitoke Yerusalemu bali limsubiri kwanza Roho Mtakatifu. Katika somo la kwanza, tunagundua kwamba idadi ya watu ndani ya kundi ilishaongezeka na kufikia watu 120 (Mdo 1:15). Hawa walikuwa wakidumu katika sala lakini bado walikuwa katika hofu ya Wayahudi. Lakini ilipotimia siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu anawatokea, ghafla wanapata nguvu, woga wote unakwisha, wanafungua milango, na kutoka nje kumhubiri Kristo bila hofu.

Ndani ya siku moja, Kanisa lilipata kutambulishwa kwa mataifa mengi. Katika Mdo 2:41, tunaelezwa kwamba mitume walipata nguvu za ajabu za kumtangaza Kristo na kwa mahubiri ya siku ya Pentekoste, waamini wapya elfu tatu waliobatizwa. Roho Mtakatifu alileta lugha ya uelewano na ya upendo kwa mitume na waamini wote. Wote wakawa kitu kimoja wakimhubiri Kristo. Hawakuwa kama wale watu wa Babeli (Mwa 11:1-9) walioishia kuwa na lugha ya mchanganyiko na kuishia kubomoa mnara wao. Walipewa umoja wa kujenga Kanisa la Kristo. Na kwa hakika waliweza kulijenga Kanisa hilo. Lugha ya upendo ndio inayojenga Kanisa la Bwana. Lugha ya upendo itusaidie kutujenga na sisi pia. Ndani ya Kanisa letu, wapo watu toka makabila mbalimbali. Kitakachotujenga ni lugha ya upendo.

Mitume walipata mafanikio makubwa kwa sababu mitume hawakuwa na lengo la kujitafutia jina kama watu wa Babeli. Watu wa Babeli waliishia kuanguka kwa sababu lengo lao lilikuwa ni umaarufu (Mwa 11:1-9). Mitume walifanikiwa kwa sababu walimtafuta Kristo. Sisi tunapaswa kuwaiga mitume pia. Tukimuacha Mungu na kutafuta umaarufu wetu sisi wenyewe, hakika tutashindwa kuleta amani yoyote ulimwenguni. Tutashindwa kuwa na lugha ya uelewano na upendo.

Ulimwengu unapaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu na siyo Sayansi au Falsafa, pale ulimwengu ulipokubali kuongozwa na Falsafa, Falsafa zimeuletea kifo na fujo. Lakini pale Roho alipoongoza, ulipata amani. Katika Mdo 2:43-47 tunaelezwa kwamba kwa kuwa Roho alikuwa ndani ya Kanisa, maisha ya Kanisa yalikuwa na utamu wa ajabu. Kila mmoja aliliona Kanisa kuwa rafiki: mfumo wao wa maisha uliwavutia wengi. Falsafa za akina Plato, Aristotle, Wastoiki na Waepikureo ziliwagawanya watu katika matabaka. Kulikuwa na tabaka la kutawala na la kutawaliwa; watu toka katika matabaka haya mawili hawakuruhusiwa kuchangamana. Kanisa la mwanzo lilimpokea kila mmoja, watumwa, viwete na maskini wote. Ukristo ulivutia idadi kubwa ya watu.

Tumshukuru Mungu aliyeliletea Kanisa Roho Mtakatifu. Tumwombe atufanye tuishi kwa amani na kila mmoja wetu. Tumwombe aendelee kuliongoza Kanisa letu na kutujalia neema. Tumwombe apambane na hali ya ulegevu ndani ya Kanisa letu atutie moto moto.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, tukiangazwa na Roho Mtakatifu, naomba nitoe ushuhuda wa Yesu kwa maisha yangu.