MEI 22, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 7 LA PASKA

Mt. Rita wa Kashia
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 28:16-20, 30-31
Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane; hata walipokutanika akawaambia, ndugu zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi asikatazwe na mtu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 11:4-5, 7

  1. Bwana yu katika hekalu lake takatifu.
    Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni,
    Macho yake yanaangalia;
    Kope zake zinawajaribu wanadamu.
    (K)Wanyofu wa moyo wauona uso wake, Ee Bwana.
  2. Bwana humjaribu mwenye haki;
    Bali nafsi yake humchukia asiye haki,
    Na mwenye kupenda udhalimu. (K)
  3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki,
    Apenda matendo ya haki,
    Wanyofu wa moyo watamwona uso wake. (K)

INJILI: Yn 21:20-25
Petro aligeuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?). Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi. Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.

TAFAKARI:
WEWE UNIFUATE MIMI: Katika Injili tunamwona Petro akimuuliza Bwana Yesu juu ya mfuasi ambaye Yesu alimpenda. Ni Yohane ambaye Petro alihisi kwamba Bwana alisema kuwa hatakufa mpaka Kristo atakapokuja. Ndipo Yesu anamuuliza hata kama atataka hayo imempasaje Petro? Mwishoni anamwambia Petro amfuate yeye tu. Na hilo ndilo jambo la msingi, kumfuata Kristo na siyo kuangalia wengine wanafanya vizuri au wanafanya vibaya. Kristo anaweka wazi kwamba tunaitwa kwa ajili ya kumfuata yeye na wala siyo kwa ajili ya kuhangaika na wengine. Si kutafuta habari za wengine, hususan mabaya yao na kuyasambaza kwa wengine. Dira yetu iwe Kristo. Tumwanagalie yeye kadiri alivyotenda nasi tujitahidi kupambana kufanya kama vile yeye alivyoishi. Katika somo la kwanza tunamwona mtume Paulo akiwa amekubali magumu anayoyapata. Hapo anapata uhuru unaomsaidia kuendelea kuhubiri na kuongea na baadhi ya Wakristo, akiendelea kuwatia moyo na hivyo kuendelea kumfuata Kristo na kutoangalia mambo mengine yasiyo ya msingi.

Sala: Tunakuomba, Mwenyezi Mungu, ututie uthabiti wa kuangalia mbele katika kazi uliyotuitia tuifanye bila ya kukatishwa tamaaa na wenzetu.